Mwanzo
Kuhusu
Huduma
Viunganishi
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Habari

TCRA: “Linda Maisha Yako ya Kidijitali; Tumia Nenosiri Madhubuti”


TCRA: “Linda Maisha Yako ya Kidijitali; Tumia Nenosiri Madhu...

 

Na Mwandishi Wetu

Kila mwaka, Alhamisi ya kwanza ya Mei, ulimwengu huadhimisha Siku ya Nenosiri Duniani. Siku hii inalenga kukuza uhamasishaji kuhusu umuhimu wa nenosiri thabiti na salama kwa ili kuweka data za watumiaji wa huduma za mawasiliano kwenye mtandao kuwa salama.

Nenosiri au Nywila ni sehemu muhimu ya mawasiliano yetu ya mtandaoni, kwa kuwa ndiyo njia ya kwanza ya ulinzi dhidi ya ufikiaji usioidhinishwa wa taarifa zetu za binafsi na nyeti zinazohifadhiwa kwenye mifumo ya mawasiliano na vifaa vya mawasiliano, vikiwemo vifaa jongefu na vinavyobebeka kama vile simu ya mkononi.

Katika zama hizi za kidijitali, ambapo tunaunganishwa kila mara kwenye intaneti na kutumia huduma mbalimbali za mtandaoni kwa mahitaji yetu ya kila siku ya mawasiliano, manenosiri thabiti ni muhimu zaidi kuliko hapo awali. Hii ni kutokana na ukweli kwamba uharamia au uhalifu kwenye mazingira ya Mtandao umeendelea kushamiri siku hadi siku licha ya jitihada zinazofanyika kukabiliana na changamoto hizo.

Kusudi kuu la nenosiri ni kuzuia ufikiaji usioidhinishwa wa akaunti zetu za mtandaoni na kuhakikisha kuwa data zetu zinasalia salama.

Hata hivyo, watu wengi bado wanatumia manenosiri dhaifu ambalo ni rahisi kukisiwa kwa urahisi, kama vile "123456" au "nenosiri," au “mwaka wa kuzaliwa” ambalo hufanya akaunti zao au taarifa zao bianafsi kuwa hatarini kwa udukuzi na mashambulizi ya mtandaoni.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inasisitiza kuwa Nenosiri thabiti linapaswa kuwa na urefu wa angalau vibambo 7 na liwe na mchanganyiko wa herufi kubwa na ndogo, nambari na herufi maalum. Pia halipaswi kuwa na maelezo yoyote ya binafsi, kama vile jina lako, tarehe ya kuzaliwa, au anwani.

Kipengele kingine muhimu cha usalama wa nenosiri ni kutumia nenosiri la kipekee kwa kila akaunti yako ya mtandaoni. Hii ina maana kwamba ikiwa moja ya nenosiri lako limeingiliwa, akaunti zako zingine bado zitaendelea kuwa salama. Baadhi ya watumiaji wa huduma za Mtandao hutumia nenosiri moja kwa vifaa vyao vyote; jambo ambalo TCRA inasema linamweka mtumiaji kwenye hatari ya kuingiliwa kwa data zake kwenye Mtandao.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa TCRA Bi Lucy Mbogoro akisisitiza umuhimu wa kutumia nenosiri (password) thabiti alisisitiza kuwa, “mbali na kutumia nenosiri thabiti na la kipekee linalofahamika kwa mtumiaji wa kifaa cha mawasiliano pekee, pia, ni muhimu kusasisha (kuhuisha) mara kwa mara nenosiri ili kupunguza uwezekano wa neno siri kufahamika na wahalifu wa mtandao, ambao hukisia na hatimae kuingilia taarifa binafsi,” alisisitiza.

Kulingana na Benedictor John, mkazi wa Dar es Salaam, watumiaji wengi hutumia nywila dhaifu kwa sababu ni rahisi kukumbuka. Hata hivyo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inasisitiza kuwa kutumia nywila imara ni muhimu kutumia nywila imara na kuihifadhi mahali salama, ili inapotokea mtumiaji ameisahau anaweza kuipata kwa urahisi na kufungua kifaa chake cha mawasiliano.

Maadhimisho ya Siku ya Nywila duniani mwaka huu, ambayo huadhimishwa kila Alhamisi ya kwanza ya mwezi Mei, yamekuja wakati ambao Tanzania imeanza kutumia rasmi Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya 2022 ambayo imeanza kutumika Mei Mosi ambapo Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Nnauye alisisitiza kuwa Sheria hiyo italinda taarifa binafsi za watumiaji wa huduma za mawasiliano kisheria. Sheria hiyo imeanzisha vitu vitatu; Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, bodi ya masuala ya taarifa binafsi na ulinzi wa faragha ya watu.

Sheria hiyo iliyopigiwa chapuo na wanaharakati wa masuala ya haki za binadamu ilisainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan Januari 31, 2023.

© 2023 TCRA, Haki zote zimehifadhiwa.