Na Mwandishi Wetu
IDADI ya usajili wa intaneti isiyohamishika Tanzania iliongezeka zaidi ya mara mbili kati ya Septemba 2025 na Septemba 2026, huku wastani wa matumizi ya data ukiwa juu zaidi, kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya hali ya sekta ya mawasiliano.
Takwimu za robo mwaka ya Julai hadi Septemba 2026, zilizotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) Mhandisi Peter Mwasalyanda zinaonesha kuwa watumiaji waliounganishwa kwa nyaya za faiba maofisini (FTTO) na nyumbani (FTTH), walitumia kiasi kikubwa zaidi cha data kwa ujumla kuliko watumiaji wa intaneti kwa vifaa vya mkononi. Vilevile wastani wa matumizi yao ulikuwa juu zaidi.
Wastani wa matumizi ya intaneti isiyohamishika ulikuwa gigabaiti (GB) 332 kwa kila usajili Septemba 2026, ikilinganishwa na GB 2.2 kwa intaneti kupitia vifaa vya mkononi. Hata hivyo, takriban asilimia 98.9 ya watumiaji wa intanegi wanapitia vifaa vya mkononi.
Taarifa iliyo tolewa na Mhandisi Mwasalyanda imebainisha kwamba matumizi ya data kwenye mitandao isiyohamishika yaliongezeka kwa asilimia 66, kutoka GB 145,253,563 mnamo Septemba 2025 hadi GB 240,570,214 Septemba 2026.
Katika kipindi tajwa, usajili wa huduma za intaneti zisizohamishika uliongezeka kwa asilimia 109, kutoka 346,296 hadi 725,270, huku usajili wa intaneti kwa vifaa vya mkononi ukiongezeka kutoka 55,972,991 hadi 63,994,431.
Usajili wa huduma zisizohamishika ulijumuisha usajili 599,176 wa watu binafsi na 126,094 wa taasisi au makampuni.
Teknolojia za faiba zinafaa sana kwa usambazaji na uhamishaji wa data kwa kasi ya juu na ujazo mkubwa, inawezesha watu kufanya kazi na mikutano.
Teknolojia hizi pia zinarahisisha maunganisho thabiti na yasiyokatika. Inawezesha pia vifaa vingi vya mawasiliano ya intaneti kuunganishwa bila kuathiri ubora au kasi.
Kwa ujumla takwimu zinaonesha kuwa usajili wa intaneti kupitia vifaa vya mkononi na mitandao isiyohamishika iliongezeka kwa asilimia 3.07 kati ya Juni na Septemba 2026, huku matumizi ya data yakiongezeka kwa asilimia 16, amebainisha Mkurugenzi Mkuu wa TCRA.
Intaneti imeenea miongoni mwa watu kwa asilimia 92.41.
Huduma za intaneti zimeleta fursa nyingi kwa watu binafsi na wafanyabiashara, ikiwemo kufanya miamala mtandaoni, masoko ya kidijitali na biashara mtandao.
Aidha zimewezesha watumiaji kujenga mitandao ya kijamii na kitaaluma. Teknolojia za kisasa pia zinawezesha uundaji na matumizi ya programu mbalimbali katika sekta tofauti.
Mitandao ya kijamii inachukua sehemu kubwa ya matumizi ya data Tanzania, huku watumiaji wengine wakitumia majukwaa hayo kutangaza bidhaa na huduma zao. Wajasiriamali wanazidi kuelekea kwenye majukwaa kama vile TikTok ili kuendeleza biashara zao.
Licha ya ukuaji huu, Tanzania inatumia asilimia 18.7 tu ya uwezo wake uliopo wa miundombinu ya intaneti ya kimataifa, ambayo ni gigabiti 17,890 kwa sekunde (Gbps).
Kupanuka kwa mitandao ya simu kumechangia kuchochea ukuaji wa intaneti ya kasi ya juu. Upanuzi huu ni pamoja na ujenzi wa minara mipya kote nchini tangu Mei 2023 ili kuweka vifaa vya mawasiliano ya kasi kuoitia teknolojia za kisasa.





