TCRA

TCRA

Creating a Level Playing Field

Initializing...
Ilichapishwa31 Julai, 2026
Ilirekebishwa:4 Agosti, 2026
Muda wa Kusomadakika 3

Tanzania yaibuka Kidedea tena Mashindano ya Hisabati Afrika

WANAFUNZI Sita wa shule za sekondari Tanzania wamenyakua jumla ya medali tisa katika mashindano ya Hisabati Afrika yaliyofanyika mwaka huu nchini Cote d’Ivoire, ambapo nchi ilishika nafasi ya tano kati ya nchi 26 zilizoshiriki, imebainika.

Shiriki Katika
Tanzania yaibuka Kidedea tena Mashindano ya Hisabati Afrika

Na Mwandishi Wetu

WANAFUNZI Sita wa shule za sekondari Tanzania wamenyakua jumla ya medali tisa katika mashindano ya Hisabati Afrika yaliyofanyika mwaka huu nchini Cote d’Ivoire, ambapo nchi ilishika nafasi ya tano kati ya nchi 26 zilizoshiriki, imebainika.

Mwenyekiti wa Chama cha Hisabati Tanzania (TMA/CHAHITA), Dkt. Said Sima, alisema jijini Dar es Salaam Jumapili, tarehe 5 Julai 2026, kuwa wavulana watatu walishinda medali moja kila mmoja huku wasichana watatu wakijishindia medali mbili kila mmoja.

Ushindi huu unaendelea kuiinua Tanzania kama kinara wa hisabati shule za sekondari, ikiwa imeshinda medali nne katika Mashindano ya Hisabati ya Afrika (PAMO) ya mwaka 2024 na idadi kama hiyo katika mashindano ya mwaka jana. Dkt. Sima alieleza kuwa Tanzania ilipanda kutoka nafasi ya 10 mwaka 2025 hadi nafasi ya tano mwaka huu.

Dkt. Sima alisema wanafunzi hao sita waliowakilisha Tanzania walichaguliwa kupitia majaribio matatu ya tathmini yaliyofuatia Mashindano ya Hisabati ya Tanzania (TAMO) mwishoni mwa mwaka 2025. Watashiriki katika Mashindano ya Kimataifa ya Hisabati (IMO) ya mwaka 2026 yatakayofanyika Shanghai, China, kuanzia tarehe 10 hadi 21 Julai 2026.

Wanafunzi watatu walioshinda medali za shaba katika PAMO ni Angel Margaret Zalwango wa Shule ya Sekondari White Lake, Sweetbert John Nene wa Ilboru, na Nyandahu Theophil Leonard wa Shule ya Sekondari Kibaha.

Medali za fedha zilikwenda kwa Lightness Pigiliano Ngiliule wa St. Francis, Joyce Pascali Sulumo wa Kilakala, na Arqam Yassir Salim wa Shule ya Rehema Wakfu.

Medali nyingine tatu zilikuwa katika kipengele maalum cha PAMO kwa wasichana. Medali hizo zilinyakuliwa na Lightness (dhahabu), Joyce (fedha), na Angel (shaba).

TMA/CHAHITA huratibu ushiriki wa Tanzania katika mashindano ya hisabati ya ndani, kikanda na kimataifa. Chama hicho kilianzishwa mwaka 1966 ili kukuza na kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa hisabati katika ngazi zote za elimu nchini Tanzania.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilifadhili washiriki hao ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kukuza masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STUH/STEM) nchini Tanzania.

TCRA inawahimiza wanafunzi wa ngazi zote - kuanzia chekechea hadi chuo kikuu - kuunda na kushiriki katika vilabu vya kidijitali ili kukuza ujuzi wa teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) na kupanua uelewa wa masuala ya kidijitali.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi Peter Mwasalyanda, aliwapongeza wanafunzi kwa utendaji wao mzuri. Alisisitiza uungaji mkono wa Mamlaka kwa matukio yanayochangia uchumi wa kidijitali na wa bluu nchini.