TCRA

TCRA

Creating a Level Playing Field

Initializing...
Ilichapishwa4 Agosti, 2026
Muda wa Kusomadakika 7

Tanzania Yaibuka Mshindi, ya Ng'ara Mashindano ya Kimataifa-Hisabati

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inazidi kuunga mkono mipango ya kitaifa inayohamasisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na masomo ya sayansi na hisabati.

Shiriki Katika
Tanzania Yaibuka Mshindi, ya Ng'ara Mashindano ya Kimataifa-Hisabati

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inazidi kuunga mkono mipango ya kitaifa inayohamasisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na masomo ya sayansi na hisabati.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi Peter Mwasalyanda, alisema mwishoni mwa wiki kuwa klabu 800 za kidijiti zimeanzishwa sehemu mbalimbali nchini na kuongeza kuwa Tanzania imezidi kuwa kinara wa hisabati Afrika na kimataifa.

Wanafunzi wa Tanzania wamekuwa wakifanya vizuri katika mashindano ya kimataifa ya hisabati ambamo TCRA inafadhili ushiriki wao, ameongeza. Mashindano hayo ni ya Olimpiki ya Hisabati ya Afrika (PAMO) na Olimpiki ya Kimataifa ya Hisabati (IMO).

TCRA inafadhili ushiriki wa Tanzania katika mashindano ya hisabati ya shule za sekondari Afrika na na Kimataifa, pamoja na klabu mashuleni zinazokuza jumuhiko la wavumbuzi wa teknolojia ya kidijiti.

Mamlaka hiyo pia inafadhili baadhi ya shughuli za Chama cha Hisabati Tanzania (TMA/CHAHITA), ambacho huratibu mashindano hayo.

Mhandisi Mwasalyanda aliwapongeza wanafunzi sita kwa kupeperusha vema bendela ya Taifa Kimataifa kwa Ushindi wao wa kipekee katika mashindano ya PAMO ya mwaka 2026 yaliyofanyika Yamoussoukro, Ivory Coast mwezi uliopita, pamoja na mashindano ya hivi karibuni ya IMO yaliyofanyika Shanghai, China.

Akiongea na wandishi wahabari walipo wasili washindi Uwanja wandege Jijini Dar Es salaam mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa Chama cha Hisabati Tanzania Dkt. Said Sima amebainisha kwamba Washiriki wa Tanzania katika mashindano ya Shanghai walipata alama za ziada, jambo lililoinua nafasi ya nchi kimataifa. Walipata alama 22 ikilinganishwa na alama 14 walizopata wawakilishi mwaka jana.

Dkt. Sima alisema Kule Shanghai, Bi. Lightness Pigiliano Ngiliule kutoka Shule ya Sekondari St. Francis alitunukiwa medali kama ‘Malkia” wa hisabati barani Afrika. Alipata taji hili akiwa Yamoussoukro.

Lightness alikuwa miongoni mwa wanafunzi sita wa Kitanzania walioshiriki shindano la hisabati barani Afrika PAMO ya mwaka huu. Wengine ni Angel Margaret Zalwango (Shule ya Sekondari White Lake), Sweetbert John Nene (Ilboru), Nyandahu Theophil Leonard (Kibaha), Joyce Pascali Sulumo (Kilakala) na Arqam Yassir Salim (Shule ya Rehema Wakfu).

Dkt. Sima ambaye ni mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Dar Ees salaam amesama Wanafunzi hao sita walishinda na kurudi nyumbani na jumla ya medali 9 katika mashindano ya PAMO kutoka Yamoussoukro, Ivory Coast , ambapo Tanzania ilishika nafasi ya 5 kati ya nchi 26 zilizoshiriki, mwezi uliopita.

Wavulana watatu walishinda medali moja kila mmoja, huku wasichana watatu wakishinda medali mbili kila mmoja katika kundi la jumla. Wasichana hao walishinda medali za ziada katika kundi maalum la wasichana.

Sayansi na Hisabati ni nguzo muhimu katika kujenga uchumi wa kidijitali. Zinapojumuishwa na teknolojia na uhandisi, masomo haya hujulikana kama STUH/STEM.

SUH/STEM ina manufaa kwa taifa na kwa wanafunzi binafsi. Mbali na kuwezesha uchumi wa kidijiti, masomo haya huwapa wanafunzi maarifa na ujuzi wa kujenga taaluma katika mazingira ya TEHAMA yanayobadilika kila mara.

Wachambuzi wanasema kuwa maendeleo ya teknolojia yataondoa ajira nyingi zilizopo sasa ndani ya miaka michache ijayo.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Mhandisi Mwasalyanda ameeleza kwamba Klabu za kidijiti, zinaanzishwa kuanzia shule ya awali hadi ngazi ya vyuo vikuu kwa madhumuni ya kuwawezesha wanafunzi kuelewa teknolojia za kidijitali na matumizi yake ya vitendo kuanzia umri mdogo.

Klabu hizi zinakuza ujuzi wa kidijitali na kujenga misingi ya utumiaji wa teknolojia ya kidijiti katika sekta mbalimbali.

Klabu hizo ni chimbuko la wavumbuzi wanao leta suluhu za Kitehama kwa changamoto mbali mbali kwa Jamii, kupitia vijana wanaoshiriki katika masuala ya STUH/TEHAMA na mawasiliano. Shughuli ndani ya klabu hizi ni pamoja na mijadala na mashindano kuhusu mada mbalimbali.

Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa Tanzania (2024-2034) unasisitiza hitaji la kuongeza ufahamu wa STUH/STEM kutoka ngazi za chini za elimu. Unawahimiza wadau kukuza ujuzi wa kidijitali na ujuzi kama vichocheo muhimu vya uchumi wa kidijitali.

Wataalamu wa elimu wanakadiria kuwa asilimia 25 pekee ya wanafunzi katika nchi nyingi za Kiafrika hufuata nyanja za kazi zinazohusiana na STUH/STEM katika elimu ya juu.

Vikwazo ni pamoja na vifaa vya kutosha, walimu wachache na dhana potofu kuhusu matatizo ya STEM. Shule nyingi hazina vifaa vya vitendo, ikiwa ni pamoja na maabara zenye vifaa.

Mhandishi Mwasalyanda alieleza kuwa mpango wa TCRA wa kuhamasisha uanzishaji klabu za kidijhiti ni sehemu ya utaratibu wake wa kuainisha mipango yake na mikakati na sera za kitaifa. Mipango hiyo ni pamoja na Mpango wa tatu wa Maendeleo wa miaka mitano, Dira ya Maendeleo Tanzania kufikia 2050 na Sera mbalimbali za Sekta ya Mawasiliano.

Alisema kuwa pamoja na vilabu, TCRA inahamasisha na kuendeleza ubunifu kwenye TEHAMA na mawasiliano kwa ujumla. Inawapatia wabunifu, bila malipo na kwa muda maalum, raslimali muhimu za mawasiliano ili kuwawezesha kujaribu miradi yao kabla ya kuanza kuitoa kama huduma.

Raslimali hizo ni pamoja na masafa ya mawasiliano bila waya, namba na misimbo, vikoa vya Tanzania kwa ajili ya huduma za intaneti na postikodi.

Shiriki Katika