
Bw. Abdallah Batenga Katunzi
Mjumbe wa BodiAbdallah Katunzi anafundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam — Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma Tanzania. Ana Shahada ya kwanza ya Sayansi ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania, Shahada ya Uzamili ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kutoka Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda. Kwa sasa, anasomea Shahada ya Uzamivu ya Habari na Mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya.
Ana uzoefu wa zaidi ya miaka 19 kama mwandishi wa habari, mwanataaluma, mtafiti na mshauri katika masuala ya Habari na Mawasiliano. Ameandika machapisho kadhaa, na ripoti yake ya utafiti ya hivi karibuni aliyoichapisha kwa ushirikiano na mtafiti mwingine iitwayo “The State of Journalism Reporting in Tanzania” ilitolewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwezi Desemba 2022.
Amekuwa mshauri mwelekezi wa masuala yanayohusu vyombo vya habari na mawasiliano akifanya kazi na mashirika ya kimataifa, yakiwemo UNESCO (Tanzania), Swiss Development Cooperation (SDC) Tanzania, africaemediterraneo lenye makao yake nchini Italia, Natural Resources Governance Institute (NRGI), Florida International Research IWASH Initiative Limited (Marekani), DW Akademie (Ujerumani), GIZ (Tanzania), Friedrich Ebert Stiftung (FES-Tanzania), Geneva Centre for Security Sector Governance (DCAF), Norwegian Church Aid (NCA), na African Centre for Media Excellence (ACME) ya Uganda.
Amekuwa mshauri mwelekezi kwa taasisi za Serikali zikiwemo Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Baraza la Wawakilishi la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET). Pia, amefanya kazi na mashirika yasiyo ya kiserikali na taasisi za vyombo vya habari, ikiwa ni pamoja na Baraza la Habari Tanzania, Tanzania Media Foundation (TMF), na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA).
Kwa sasa anasimamia mradi wa utafiti wa vyombo vya habari nchini unaojulikana kama “Mradi wa Ubora wa Maudhui ya vyombo vya Habari Tanzania” (https://sjmc.udsm.ac.tz/yearbook/ ), mradi huu unachunguza ubora wa uripoti wa vyombo vya habari kila mwaka nchini. Mwezi Mei 2023, alitunukiwa tuzo ya mshindi wa kwanza kwenye kipengele cha tafiti zilizofikia wadau wengi (outreach research project) kwenye maonyesho ya nane ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mwaka 2022 alikuwa Mratibu wa Kitaifa wa Siku ya Redio ya Umoja wa Mataifa nchini iliyoadhimishwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.