USULI NA HISTORIA
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ni taasisi iliyoasisiwa kwa mujibu wa sheria yenye wajibu wa kudhibiti sekta ya mawasiliano ya Kielektroni na Posta Tanzania. Ilianzishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) namba 12 ya mwaka 2003, ambayo iliunganisha zilizokuwa Tume ya Mawasiliano Tanzania (TCC) na Tume ya Utangazaji Tanzania (TBC).
TCC ilianzishwa 1993 na kupewa nguvu za kisheria kusimamia huduma za mawasiliano ya simu na Posta. Tume ya Utangazaji Tanzania (TBC) pia ilianzishwa 1993 na kupewa nguvu za kisheria kusimamia sekta ya utangazaji.
Kutokana na maendeleo ya teknolojia, umuhimu wa kuleta ufanisi kwenye utoaji wa huduma za Serikali kwa umma na kupunguza ukiritimba, kulikuwa na umuhimu wa kuunganisha tume mbili za usimamizi, TCC na TBC na kuunda Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) mwaka 2003.
Mamlaka ilianza shughuli zake tarehe 1 Novemba 2003 ikichukua majukumu ya tume mbili zilizounganishwa. Majukumu ya TCRA yameainishwa kwenye Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ya mwaka 2003, Kifungu cha 4 (1) hadi (7).