Mha. Peter P. Mwasalyanda
Mkurugenzi MkuuWapendwa Wadau,
KAMA SEHEMU YA MKAKATI wa kujenga jamii inayowezeshwa na huduma za mawasiliano, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inafanya kazi kwa kuzingatia Dira yake ya: “Jamii iliyowezeshwa na huduma za mawasiliano jumuishi na endelevu.” Tunaendelea kukuza upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wote na zilizo salama, nafuu, zenye ubora na zinazopatikana kila wakati.
TCRA inaendelea kuzingatia mabadiliko ya kasi ya teknolojia katika Sekta ya Mawasiliano. Kwa kuzingatia hilo, TCRA imesawanisha shughuli zake na Malengo ya Maendeleo ya Kitaifa, pamoja na yale ya Kikanda. Masuala muhimu ya maendeleo ya kitaifa, kikanda na kimataifa yanayopewa kipaumbele na TCRA ni pamoja na Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali Tanzania 2024 - 2034, Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 na Sera za kisekta, kama vile, Sera ya Taifa ya TEHAMA, Sera ya Taifa ya Habari na Utangazaji na Sera ya Taifa ya Posta. Vyote hivi vimewezesha mabadiliko ya kidijitali na fursa zaidi katika Sekta ya Mawasiliano, Utangazaji na Posta. Haya yote yanabeba maono imara ya kujenga Taifa lenye uwezo na linalotegemea teknolojia za habari na mawasiliano (TEHAMA) ili kujenga mustakabali imara wa kidijiti. Vile vile, yanawezesha matumizi yenye uwajibikaji ya teknolojia zinazoibukia, ikiwa ni pamoja na Akili Unde (AI). Malengo ya Kimataifa ya Maendeleo Endelevu (SDGs) 2030, Ajenda ya Afrika 2063 na utambuzi wake wa nguvu ya TEHAMA katika kuleta mabadiliko ni miongoni mwa vichochezi vingine vya azma yetu. TCRA pia inatekeleza ajenda ya Uendelevu na Mazingira, Kijamii na Utawala (ESG). Hii inalenga kukuza ukuaji wa Sekta ya Mawasiliano wenye uwajibikaji na ulio endelevu kimazingira.
TCRA inakuza ushirikishwaji kwa kukuza na kuunga mkono ubunifu kwa Tanzania iliyounganishwa na iliyojumuishwa kidijitali. Mpango wetu wa vilabu vya kidijiti, Wasichana katika TEHAMA kwenye Shule na Taasisi za Elimu ya Juu unalenga kukuza TEHAMA na matumizi yake kuanzia umri mdogo.
Kuenea kwa Teknolojia ya mawasiliano ya simu uzao wa tano (5G) sio tu umeshuhudia mabadiliko katika Sekta ya Mawasiliano nchini hasa kwenye ufanisi wa utendaji katika miradi ya kimkakati ya kitaifa kwa mfano Reli ya Kisasa (SGR), bali pia umefungua fursa mpya kwa wawekezaji. Hii imewezesha kuwepo huduma na bidhaa mpya sokoni.
Tunaendelea kuhakikisha uwepo wa huduma za mawasiliano zilizo salama, nafuu, zenye ubora na za uhakika ili kutimiza dhamira yetu ya kusimamia huduma za mawasiliano kwa ustawi wa jamii ya kitanzania. Uwezeshaji wa watumiaji wa huduma za mawasiliano, unabaki kuwa kipaumbele kikuu kinachoungwa mkono kupitia programu za uhamasishaji kwa umma na elimu zinazolenga kuongeza ujuzi wa kidijitali na matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano.
TCRA ina nia ya dhati ya kuibadilisha Sekta ya Simu & Intaneti, Utangazaji na kuimarisha miundombinu ya Posta na Usafirishaji Vifurushi ili kukidhi mahitaji yanayotokana na ongezeko la huduma za kielektroniki na programu tumizi za kidijitali.
Tunatilia maanani ustawi, maendeleo ya kitaaluma na uboreshaji wa ujuzi wa wafanyakazi, kuhakikisha wana afya na uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa weledi zaidi na kukidhi matarajio ya umma, huku tukizingatia mabadiliko makubwa ya kiteknolojia tunapotekeleza majukumu ya usimamizi wa Sekta ya Mawasiliano.
Tutaiwezesha Tanzania kutumia TEHAMA ili kuendeleza uendelevu wa mazingira na ustahimilivu wa hali ya hewa, na kuendelea kutekeleza ajenda ya kimataifa ya kidijitali na kuendeleza mafanikio ya nchi. Haya ni pamoja na Tanzania kutambuliwa kimataifa kama mfano wa kuigwa wa daraja la kwanza katika usalama wa mtandao. Tutaendeleza mitandao ya mawasiliano ya kasi na huduma kwa wote, ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya usalama na ulinzi wa watoto mtandaoni.
TCRA inathibitisha azma yake ya kutoa huduma za usimamizi za ubora wa juu kupitia utaratibu wa kushirikisha wadau. Kwa kuzingatia kanuni ya “usimamizi kwa kushirikisha na kushauriana, tunashirikisha kikamilifu wadau katika kubuni, kuanzisha na kutekeleza mifumo bora ya usimamizi, iliyo jumuishi na yenye ufanisi.
Ninawatakieni kila la heri.
Mhandisi Peter P. Mwasalyanda,
MKURUGENZI MKUU