Sekta ya mawasiliano yakua kwa kasi

KUMEKUWA na kukua kwa kasi kwa sekta ya mawasiliano nchini ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa laini za simu za mkononi zilizosajiliwa kutoka 48,939,530 Julai mwaka 2020 hadi 53,063,085 Aprili 2021; sawa na ongezeko la asilimia 10.8.
Akiwasilisha Bungeni, jijini Dodoma makadirio na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2021/2022 hivi karibuni, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile amesema idadi ya watumiaji wa huduma za intaneti imeongezeka kutoka 26,832,089 Julai mwaka 2020 mpaka 29,071,817 Aprili 2021; sawa ongezeko la asilimia 8.3.
Aidha, amesema akaunti za matumizi ya huduma za pesa kupitia simu za mkononi zimeongezeka kutoka 27,127,298 Julai mwaka 2020 mpaka 32,720,180 Aprili, 2021; sawa na ongezeko la asilimia 20.6.
Mhe. Waziri Dkt. Ndugulile amewaambia Wabunge kwamba vituo vya redio vimeongezeka kutoka 193 Julai mwaka 2020 mpaka 200 Aprili 2021. Aidha Televishen zimeongezeka kutoka 43 Julai mwaka 2020 hadi 50 Aprili 2021.
Jumla ya shilingi Shilingi 170,513,110,859,867 zilitumwa na kupokelewa kupitia huduma za pesa kwa njia ya simu za mkononi kati ya tarehe 1 Julai 2020 na 30 Aprili 2021; kwa mujibu wa mfumo wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania wa kusimamia na kuratibu mawasiliano ya simu (TTMS).
Kuongezeka kwa miundombinu muhimu ya mawasiliano nchini ni kielelezo tosha na ushahidi wa kuboreshwa kwa utoaji wa huduma; jambo ambalo linachangia kuongeza kipato na kuboresha hali ya maisha ya wananchi.