JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

CHETI CHA TAKA ZA KIELEKTRONIKI

UKAGUZI WA AWALI WA VIFAA VYA MAWASILIANO VYA KIELEKTRONIKI NA UKUSANYAJI WA ADA KATIKA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Namba 12 ya 2003, kwa lengo la kusimamia mawasiliano nchini Tanzania.

TCRA imebaini ongezeko kubwa la matumizi ya programu na huduma za mawasiliano ya kielektroniki duniani kote, jambo ambalo limepelekea kuongezeka kwa idadi ya vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki. Vifaa hivi vinaweza kuwa na viambata hatari ambavyo vinaweza kuathiri mazingira na afya ya binadamu endapo havitasimamiwa vizuri, hivyo kuna haja ya kusimamia kwa ufanisi ili kuzuia madhara yanayoweza kutokea. Ongezeko la kasi ya vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki visivyokuwa na uangalizi linaleta tishio kwa ustawi wa mazingira na afya ya binadamu.

Tanzania ni miongoni mwa nchi iliyoridhia Mkataba wa Basel chini ya Umoja wa Mataifa. Lengo kuu la mkataba huu ni kulinda afya ya binadamu na mazingira dhidi ya athari mbaya zinazotokana na harakati za kimipaka na usimamizi wa taka hatari, zikiwamo taka za kielektroniki. TCRA imepewa jukumu la kulinda maslahi ya watumiaji wa mawasiliano, hususani usalama wao wanapotumia vifaa vya kielektroniki. Hivyo basi, TCRA iliingia mkataba na M/S Bureau Veritas Tanzania Limited kutekeleza mchakato wa ukaguzi wa ukusanyaji wa ada ya awali kwa vifaa vyote vya mawasiliano ya kielektroniki vinavyoingizwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Programu ya ukusanyaji wa ada hizi ilianza rasmi tarehe 23 Mei, 2023.

Vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki vinavyoingizwa nchini lazima vifanyiwe ukaguzi na kulipa ada ya awali, itakayoshughulikia mchakato wa mwisho wa maisha ya vifaa husika, pamoja na usimamizi wa taka za kielektroniki, kwa mujibu wa Mkataba wa Basel na kama inavyotakiwa na Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta kuhusu Ubora wa Vifaa vya Mawasiliano ya Kielektroniki na Usimamizi wa Taka za Kielektroniki za mwaka 2020.

Wazalishaji na wasambazaji wa vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki waliopo nje ya nchi wanawajibika kuhakikisha kuwa vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki vinavyoingizwa Tanzania vinakidhi matakwa ya Kanuni ya 17(1)(a) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta Kuhusu Ubora wa Vifaa vya Mawasiliano na Usimamizi wa Taka za Kielektroniki za mwaka 2020, pamoja na kutekeleza programu ya ada za vifaa hivyo.

Waingizaji au waagizaji wa vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki lazima wahakikishe kuwa vifaa vinavyoingizwa nchini vimelipiwa ada na vimepata cheti cha idhinisho.

Ili kuwasilisha maombi ya cheti cha idhinisho kwa vifaa vyako vya mawasiliano ya kielektroniki, tafadhali tembelea https://verigates.tcra-bureauveritas.co.tz/

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!