JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

WANNE WAIBUKA WASHINDI, SHINDANO LA CYBERCHAMPIONS 2025


WANNE WAIBUKA WASHINDI, SHINDANO LA CYBERCHAMPIONS 2025

Na mwandishi wetu - Dodoma

VIJANA Wanne kati ya mia sita (600) wameibuka washindi wa shindano la CyberChampions mwaka 2025. Shindano hilo linaloandaliwa na kuratibiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania – TCRA, limehusisha vyuo zaidi ya 40 na washiriki mia sita kutoka vyuo vya elimu ya juu mbalimbali nchini.

Vijana hao ni Amani Nsemwa kutoka chuo kikuu cha Dodoma (UDOM), Julius Mpagama kutoka Chuo Kikuu Katoliki Ruaha (RUCU), John Mange kutoka Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) na Rebeca Kubanda kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Akizungumza wakati wa kutoa tuzo kwa washindi wa shindano hilo Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Jabiri Bakari amewataka vijana kutumia fursa zinazopatikana kwenye teknolojia ya habari na mawasiliano duniani na kujikita katika uvumbuzi wa kidijitali.

Dkt. Jabiri amesema zipo fursa nyingi ambazo zinapatikana kwenye mitandao kama vijana watatumia fursa hizo kujipatia kipato na kuchochea maendeleo ya Uchumi wa kidijiti.

"Zipo fursa nyingi ambazo zinapatikana kwa kutumia teknolojia ya kidigiti kwa hiyo jaribu kuingiza pesa kwa kutumia bando" amesema Dkt. Bakari.

Ameongeza kuwa uchumi wa kidijiti hauhitaji mtu kuwa na fedha nyingi au mtaji mkubwa ila kinachotakiwa ni kutumia akili kwa kutengeneza program tumizi ambazo zinasaidia kutatua changamoto kwenye jamii inayowazunguka.

Amesema dunia ya sasa inakwenda kidigitali hivyo ni lazima vijana wafundishwe fursa zinazopatikana huko kuanzia ngazi ya elimu ya awali hadi vyuo vikuu kwa kuunda klabu za kidigiti ambazo zitawawezesha kujua fursa na kuzitumia kwenye ulimwengu wa digitali.

Shindano la CyberChampions linaratibiwa na TCRA kwa lengo la kuibua, kuimarisha na kukuza uwezo kwa vijana kukabili vihatarishi vya usalama mtandaoni na kushiriki kikamilifu kwenye Uchumi wa kidjiti.

Shindano la CyberChampions ambalo awali lilifahamika kama CyberStars linafanyika kwa awamu ya sita mfululizo likihusisha vijana kutoka katika taasisi za elimu ya juu. Kwa mwaka 2025 kumekuwa na idadi kubwa ya waliojiandikisha kushiriki kulinganisha na miaka iliyopita na hivyo kutoa hamasa kwa waandaaji kufikiri zaidi katika masuala ya Usalama mtandaoni na kuendelea kuandaa mashindano haya kwa namna ya tofauti na katika ubora wa hali juu zaidi. 

Mchakato wa kupata washiriki huanza kwa tangazo la usajili na taarifa nyingine muhimu kuhusu shindano ambazo hutolewa kupitia kurasa za mitandao ya kijamii za TCRA Pamoja na tovuti ya www.tcra.go.tz.

Baadhi ya washiriki wa shindano hilo wameipongeza TCRA kwa kuandaa shindano hilo na kuwaongezea ujuzi kwenye eneo la usalama mtandaoni huku wakitoa wito kwa vijana wengine kujitokeza kushiriki kwenye shindano la CyberChmapions kwa miaka mingine.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo. Mshindi wa tatu wa shindano la cyberchampions 2025 Bw. Julius Mpagama amesema shindano hilo limewajengea uwezo na kujua mambo mengi kuhusu mtandao wa kidigitali ambayo walikuwa hawayajui.

Aidha amesema suala la kuanzisha klabu za kidigiti kwenye vyuo vyao litapewa kipaumbele ili kila kijana ajue fursa zinazopatikana kwenye ulimwengu wa kidigitali tofauti na wanavyojua kwa sasa.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!