5G yazidi kujikita Tanzania

Uwekaji wa vifaa vya teknolojia ya uzao wa tano wa mawasiliano ya mkononi (5G) kwenye minara uliongeka kwa asilimia 38 na kuenea huduma kupitia teknolojia hiyo kuliongezeka kwa asilimia 195 kati ya Juni 2024 na Juni mwaka huu, imefahamika.
Takwimu za hali ya mawasiliano kufikia Juni 2025 zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonesha kwa 5G ilienea kwa kwa asilimia 5.9 miongoni kwa watu Juni 2025 kutoka asilimia 2 Juni mwaka jana. Ilienea kwa asilimia 3.6 ya watu Machi mwaka huu.
Teknolojia hiyo imefika asilimia 26 ya eneo la Tanzania, kutoka asilimia 15 Juni 2024 na 23 Machi mwaka huu.
Vifaa kwenye minara inayowezesha mawasiliano ya 5G iliongezeka kwa asilimia 38, kutoka 754 Juni 2024 hadi 1,038 Juni mwaka huu.
Uwekaji vifaa vya teknolojia hiyo uliongezeka kwa kati ya asilimia 76 na 116 katika mikoa mitatu. Huku mikoa yote ikiwa na angalau minara miwili yenye vifaa hivyo.
Ongezeko kubwa lilikuwa asilimia 116 mkoa wa Pwani, kutoka minara sita yenye vifaa hivyo Juni 2024 hadi 13. Mkoani Mwanza viliongezeka kwa asilimia 100, kutoka 23 hadi 46 na Mjini Magharibi kwa asilimia 76, kutoka 37 hadi 65.
Mikoa inayoongoza kwa minara na vifaa vinavyowezesha 5G na idadi yao kwenye mabano ni Dar es Salaam (688), Dodoma (50) Mjini Magharibi (65), Mwanza (46), Arusha (37), Mbeya (19), Morogoro, Songwe, Pwani (13) na Kilimanjaro (11).
Teknolojia ya 5 G iliingia Tanzania mwaka 2022. Ina kasi kubwa, ufanisi na inaamimika zaidi kwenye mawasiliano ya kasi. Vilevile inawezesha kuunganishwa kwa wakati mmoja watumiaji wengi na vifaa vingi vya mawasiliano.
Taarifa ya hali ya mawasiliano nchini imekuja sambamba na kukamilika kwa mchakato wa utoaji wa masafa ya mawasiliano ya kasi kwa watoa huduma kwa njia ya ushindani. Masafa hayo, kwenye wigo wa bendi ya megahezi (MHZ) 3600 mpaka 3800 yalitolewa na TCRA kwa njia ya ushindani tarehe 10 Julai mwaka huu.
Masafa hayo yanawezesha matumizi ya teknolojia za habari na mawasiliano (TEHAMA) za kisasa kwenye sekta zote.
Watoa huduma watatu kati ya watano wa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi waliwasilisha dau, kushinda na kupewa leseni za matumizi ya masafa hayo. Walioshinda ni Halotel, Yas na Vodacom.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt Jabiri Bakari amesema wamewapa washindi masharti ya kuweka miundombinu na kueneza huduma sehemu zote Tanzania. Lengo ni kuhakikisha kuwa watumiaji wanaunganishwa na kufaidika kikamilifu na upatikanaji wa huduma zinazotumia masafa yanayowezesha mawasiliano ya kasi.
Dkt Bakari alieleza kuwa kuenea kwa mitandao na huduma kupitia masafa hayo vitawezesha kukuza sekta nyingine na kuharakisha ujenzi wa uchumi wa kidijiti Tanzania.
Taarifa hiyo imesema ueneaji wa teknolojia za uzao wa tatu (3G) na wa nne (4G) uliongezeka kwa kati ya asilimia 11 na tano kati ya Juni 2024 na Juni mwaka huu. Kuenea kijiografia nchini kuliongezeka kwa asilimia 8.7 katiya Juni 2024 na Juni 2025.
Uzao wa tatu umeenea miongoni mwa watu asilimia 93.4 ya watu, kutoka 89 na uzao wa nne asilimia 92 kutoka 83 kipindi hicho. Kuenea 3G kijiografia ni asilimia 75, kutoka 73 na 4G asilimia 75, kutoka 69.