JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Kuelekea Sera ya Huduma za Pamoja Afrika


Kuelekea Sera ya Huduma za Pamoja Afrika

 

Sekta ya Posta kuwa ya Kidijitali   

CHOMBO cha pamoja cha sekta ya Posta Afrika, yaani Umoja wa Posta Afrika (PAPU) kimejizatiti kuwa na sera moja na Kanuni zinazofanana kama sehemu ya mkakati wa kuhakikisha maendeleo endelevu ya huduma za Posta barani la Afrika.

Katika ujumbe wake kwenye sherehe iliyofana ya kukaribisha uongozi mpya wa PAPU mjini Arusha hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Dkt. Jabiri K. Bakari amesema Umoja huo unaendelea kuwa kituo kikuu cha kujenga ENEO MOJA LA POSTA AFRIKA kwa lengo la kuboresha viwango vya maisha vya wananchi na maendeleo ya nchi wanachama.

Amesema kuanzisha mifumo ya kidijitali za utoaji wa huduma za za Posta ni mojawapo ya majukumu ya msingi ya PAPU ili kufungua fursa na kuendeleza shughuli za biashara mtandaoni sio tu kwa Afrika bali pia kufungua fursa za Afrika kufanya biashara dunia nzima.

“Mchango wa huduma za Posta katika kujenga uchumi wa kidijitali na kuenea kwa kasi kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano vinatoa fursa pekee ya kuendeleza huduma za Posta Afrika”, aliongeza. Hotuba yake iliwasilisha na mwakilishi wake, Dkt. Emmanuel Manasseh wa TCRA.

Dkt. Jabiri aliwapongeza viongozi wa PAPU wanaoingia madarakani na wale waliomaliza muhula wao.

Dkt. Bakari  alieleza kwamba ujenzi wa jengo la makao makuu ya PAPU, litakalokuwa na ghorofa 17 mjini Arusha kwa ubia na TCRA ni kielelezo cha ushirikiano imara na wa muda mrefu wa taasisi hizo.

Alifafanua kwamba mchakato wa kuboresha sekta ya posta kunahitaji majadiliano ya kina, ushirikiano endelevu, kujenga imani na kubadilishana uzoefu miongoni mwa nchi wanachama wa PAPU.

Katika hotuba yake, aliyekuwa Waziri Wamawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile (Mb) alisema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuunga mkono kwa dhati mipango ya kuwa na mifumo ya utoaji wa huduma za Posta zinazofanana Afrika.

“Serikali imejizatiti kuhakikisha kwamba inaendela kuiunga mkono PAPU, kukiwezesha chombo hiki kuwa cha huduma Kisasa za Posta ambazo ni imara, cha kisasa na kinachotumia TEHAMA kwa lengo la kuboresha viwango vya maisha ya watu na maendeleo endelevu ya

nchi wanachama  wa PAPU”, alisema Dkt. Ndugulile.

Aliongeza kwamba jengo la kisasa la ofisi na uwekezaji ni ushahidi wa azma ya Serikali kuifanya PAPU iwe chombo cha bara zima la Afrika kitakachozalisha mapato na cha kuaminika.

Dkt. Ndugulile aliwapongeza viongozi waliomaliza muhula wao na wanaoingia madarakani, Bwana Younouss Djibrine na Dkt. Sifundo Chief Moyo wa Zimbabwe na Naibu Katibu Mkuu anayendoka, Bw.  Mr Kolawole Raheem Aduloju na anayeingia, Bi. Jessica Uwera SSengooba wa Uganda.    

Waziri Dkt. Jenfan Muswere wa Zimbabwe aliishukuru Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sio tu kwa kuwa mwenyeji wa PAPU tangu Umoja huo ulipoanzishwa mwaka 1980 bali pia kwa kuendelea na nia njema ya kuunga mkono PAPU bila bila kuyumba, kifedha, hali na mali. 

Waziri wa Zimbabwe wa TEHAMA, Posta na Usafirishaji wa Vifurushi na Vipeto, Mhe. Dkt. Jenfan Muswere, ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye sherehe hiyo alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za kuboresha shughuli za Umoja huo.

Aliutaka uongozi mpya kuhakikisha kwamba utekelezaji wa majukumu ya PAPU unazingatia Mkakati wa Posta Duniani uliopitishwa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Posta Ulimwenguni (PAPU), jijini Abidjan hivi karibuni.

Dkt. Muswere alisisitiza kuwa Zimbabwe itaendelea kuunga mkono uendeshaji wa PAPU kwa ufanisi ili kuwezesha upatikanaji wa huduma bora kwa nchi zote wanachama. Hili litafanikiwa kwa kuwa na sera na kanuni zinazofanana kwa lengo la maendeleo ya Afrika kupitia sekta ya Posta ya kidijitali.

PAPU ni chombo mahsusi cha Umoja wa Afrika (AU) kwa masuala ya Posta. Kilianzishwa tarehe 18 Januari 1980 kufuatia uamuzi wa Mkutano Mkuu wa nchi 35 wanachama wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) uliofanyika Arusha kuanzia tarehe 8 hadi 18 Januari mwaka huo.

Umoja huo ulianzishwa kwa lengo la kuratibu shughuli zote za kuendeleza huduma za Posta Barani Afrika. Hivi sasa una wanachama 45.

Miaka ya themanini, aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano na Ujenzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na ambaye mwaka 1990 aliteuliwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Mhe. John S. Malecela alihakikisha kwamba PAPU inapatiwa kiwanja Sekei, karibu na eneo maarufu la Philips, mjini Arusha.

Ndoto ya kujenga jengo la pamoja la ofisi na uwekezaji ilianza miaka ya tisini kupitia iliyokuwa Tume ya Mawasiliano Tanzania (TCC), Shirika la Posta Tanzania (TPC) na Shirika la Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTCL). Taasisi hizi zilikubaliana kuwekeza kwa pamoja na PAPU kwenye jengo la kisasa; kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa kwanza wa TCC, Mhandisi Emmanuel Ole Kambainei.

Maono hayo yamefanyiwa kazi, na TCRA, chini ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inashirikiana na PAPU kwenye mradi huu wa ubia, ambao utekelezaji wake umezalisha  mamia ya ajira.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!