JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Watumiaji Huduma za Mawasiliano Watakiwa Kujilinda Mtandaoni


Watumiaji Huduma za Mawasiliano Watakiwa Kujilinda Mtandaoni

 

Watumiaji wa huduma za mawasiliano wametakiwa kulinda taarifa zao za binafsi na kuwa makini katika matumizi ya nywila na namba ya siri inayotumika kwenye miamala ya kifedha ili kujihakikishia usalama mitandaoni.

Afisa Mwandamizi Mkuu wa Mamlaka ya MawasilianoTanzania (TCRA), Bwana Semu Mwakyanjala wamesema ingawaje Watanzania wengi wanatumia huduma za mawasiliano kwa kuzingatia sheria na kanuni, kuna wachache ambao wanafanya uhalifu kama vile utapeli, ulaghai na wizi wa taarifa na fedha za watumiaji.

Afisa huyo, alikuwa wanatoa elimu kwa wananchi kwenye gulio lililopo kijiji cha Kalinzi mkoani Kigoma Jana, ikiwa ni sehemu ya mpango kabambe wa TCRA wa kuongeza kiwango chauelewa wa wananchi na watumiaji kwenye masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na umuhimu wa matumizi sahihi na salama ya mtandao.

Bwana Mwakyanjala amesisitiza kwamba nywila na namba ya siri visitolewe kwa mtu mwingine kwa namna yoyote ile. Aidha aliwashauri watumiaji kuchagua nywila ambazo zinachanganya maneno na tarakimu na kubadilisha nywila hizo mara kwa mara.

Nywila ni maneno, herufi au mchanganyiko wa hivi vyote ambavyo mtumiaji wa vifaa vya kidijitali anaweka ili kuzuia kifaa chenyewe, kazi iliyohifadhiwa kwenye kifaa hicho au akaunti ya barua pepe au miamala la kielektroniki visiingiliwe na mtu asiyehusika.

Kutokana na kukua kwa matumizi ya vifaa vya kielektroniki, matumizi ya nywila yanaongezeka, sambamba na uhalifu wa watu kuingilia nywila za watu wengine.

Afisa huyo wa TCRA, amewashauri watumiaji kuwa makini na kuchagua aina ya taarifa wanazowekwa kwenye mitandao ya jamii kwani zinaweza kutumiwa vibaya na wahalifu.

Aliwataka watumiaji kuwa makini wanapopigiwa simu na watu wanaowataka kutoa namba zao za siri, au taarifa zao binafsi, hata kama anayepiga anadai anatoka mtandao wanaotumia.

“Mawasiliano kati ya Mtoa huduma na Mtumiaji wa huduma za Mawasiliano ni namba mia moja tu (100). Ukipigiwa simu na namba yoyote usitekeleze maagizo, ila tuma namba hiyo ya tapeli au ujumbe ujumbe wake kwenda namba “15040” ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya hao wahalifu. Namba hiyi ni bure, hailipiwi”, alisisitiza-Bw. Mwakyanjala.

Mkoa wa Kigoma unaongoza kwa kilimo cha michikichi ambayo inazalisha mafuta ya mawese. Mwakyanjala aliwataka wakazi wa mkoa huo kutumia mawasiliano, kutafuta masoko ya mazao yao.

Wakitoa maoni yao, wafanyabisahara wa zao hilo; wameshukuru Serikali, kupitia TCRA kwa hatua zinazofanyika kuboresha mawasiliano mkoani Kigoma na kufungua fursa za kutafuta masoko,kuuza kirahisi, kujiongezea kipato na kuboresha maisha.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!