Sheria ya Ulinzi wa Data, Faragha yaiva; Sasa kuwasilishwa Bungeni
Hatimaye, baada ya kusubiriwa kwa muda mrefu, Muswada wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi unatazamiwa kusomwa kwa mara ya kwanza Bungeni mwezi huu, Serikali imeweka bayana Jumatano, 8 Septemba 22 2022 .
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Nnauye (Mb) alieleza hayo jijini Dar es salaam pembezoni mwa Kongamano la TEHAMA liitwalo Connect 2 Connect na kubainisha kuwa kuwasilishwa kwa Muswada huo kabla ya kusainiwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa sheria kamili kutatoa hakikisho la usalama wa data na taarifa binafsi za watumiaji huduma za mawasiliano kwenye mtandao.
"Baraza la Mawaziri limeturuhusu rasmi kuendelea na mchakato huu," alibainisha Waziri Nnauye. Alieleza kuwa katika utekelezaji wa Sheria hiyo, Tanzania itakopa uzoefu wa nchi nyinginw ambazo tayari zina Sheria kama hiyo. Kwa kufanya hivyo, alifafanua, nchi itaweza kutatua changamoto zinazohusiana na sheria na hivyo kuifanya kuwa rafiki kwa watumiaji.
"Kadiri shughuli nyingi za kijamii na kiuchumi zinavyofanyika mtandaoni, umuhimu wa faragha na ulinzi wa taarifa binafsi unazidi kutambuliwa na kuongezeka. Tunalazimika kuwezesha data zetu kuwa salama,” alibainisha Mheshimiwa Nnauye.
Changamoto za kimtandao zinazohusisha kuvuja kwa taarifa binafsi ilibainika kuwa zinahusisha watumiaji wa huduma za kimtandao kukusanya, kushirikisha habari na taarifa zao binafsi na za watu wengine bila idhini ya watumiaji, hivyo kuongeza changamoto ya kuvuja kwa taarifa.
Ilibainika pia kwamba, baadhi ya watu hukabiliwa na unyanyasaji wa kimtandao unaosababisha matokeo hasi yakiwemo kujinyonga kutokana na maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), suala ambalo Serikali ya Tanzania imejidhatiti kulikabili kupitia uwepo wa Sheria hiyo.
"Tunalenga pia kuangalia maadili ya matumizi ya mtandao kwa kiwango ambacho matumizi hayo yanaweza kuwa chini ya uangalizi," alisisitiza na kuongeza: "Tabia ya kutowajibika mtandaoni ni muhimu idhibitiwe."