JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

EACO kuwezesha upatikanaji wa ‘Smartphone’ kwa Mtumiaji


EACO kuwezesha upatikanaji wa ‘Smartphone’ kwa Mtumiaji

 

Shirikisho la Taasisi za TEHAMA Afrika Mashariki (EACO) linatekeleza mpango wa upatikanaji wa simu janja ‘smartphone’ za bei nafuu zitakazowafikia wananchi hasa wa kipato cha kawaida kwenye nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Akizungumza wakati wa hitimisho la kikao cha Ishirini na Nane cha Kamati Kuu ya Utendaji ya Shirikisho la Taasisi za TEHAMA Afrika Mashariki (EACO) na kufanyika jijini Dar es salaam kujadili hatua za ukuzaji sekta ya Mawasiliano katika ukanda wa Afrika Mashariki, Mtendaji Mkuu wa EACO Dkt. Ally Simba amesisitiza kuwa taasisi hiyo inasimamia mpango huo kwa dhati ili kuhakikisha wananchi katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanatumia teknolojia ya kisasa ya Mawasiliano.

Akizungumzia mpango wa kuhamasisha matumizi ya simu janja katika ukanda huo, Simba amebainisha kuwa, EACO kwa sasa inatekeleza mpango ujulikanao kama “Mpango wa Simu Janja Rahisi’’ ambao unalenga kuwezesha idadi kubwa zaidi ya watumiaji wa teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Kwa kuwa watu wengi hawana uwezo wa kupata kompyuta mpakato ‘lap top’ kwa hiyo smartphone inakuwa kama mwokozi, hata wanafunzi wanatumia simu janja kujisomea, hivyo kupatikana kwa simu janja tunadhani kuwa ni kipengele muhimu kitakachosaidia kukua kwa matumizi ya TEHAMA katika ukanda wa Afrika Mashariki”.

Mtendaji huyo Mkuu wa EACO amesisitiza kuwa nchi wanachama wa taasisi hiyo ambazo ni Tanzania, Kenya,Rwanda,Uganda,Sudani Kusini na Burundi zimeweka mkakati wa pamoja kuhakikisha zinakuza  TEHAMA kwa kutambua mchango chanya wa sekta hiyo katika kukuza uchumi.  

Katika kuhakikisha mpango wa kufikisha smartphone nafuu kwa kila nchi mwanachama EACO imesisitiza kuwa tayari imeanza utekelezaji wake nchini Rwanda kwa kuvishirikisha vyama vya ushirika ambapo wananchi wenye nia ya kupata simu hizo wapatao Sitina na Tano elfu wamejiandikisha na wanahakikiwa.

Simba ameongeza kuwa wabia wanne tayari yameonyesha nia ya kuunga mkono mpango huo na tayari wamekutana na EACO kwa makubaliano; wabia hao ni mabenki ambayo yatatoa huduma za kifedha, kampuni za bima ambazo zitatoa huduma ya bima ikiwa mtumiaji wa simu atapata dharura itakayosababisha simu hiyo kutotumika, wauzaji wakubwa wa simu ambao watawezesha upatikanaji wa simu kwa bei punguzo kwa mtumiaji wa mwisho wa smartphone, pamoja na kampuni za mawasiliano ya simu.

Akibainisha manufaa ya matumizi ya simu janja amesisitiza kuwa sekta ya kilimo itanufaika katika eneo la Afrika Mashariki kwa kuwa simu janja ni nyenzo muhimu kwa wakulima kwani huweza kutumika kuratibu mitambo ya umwagiliaji na kupata taarifa za ughani.

Amebainisha kuwa simu hizo zitapatikana baada ya benki kutoa mkopo ambapo mtumiaji atakuwa akilipa kwa awamu hadi atakapokamilisha deni la simu yake, huku akibainisha kuwa wananchi wengi kwenye ukanda wa Afrika Mashariki wamekuwa wakishindwa kupata simu janja kutokana na uwezo mdogo hivyo mpango huo utakuwa mwokozi.

Kwa kadri simu janja ya bei ya chini yenye ubora stahiki inaweza kupatikana angalau kwa Dola 50 hivyo mtumiaji wa mwisho ikiwa ataipata simu hiyo kwa mkopo atalazimika kulipa kiasi cha angalau dola 6 sawa na kadri ya shilingi 13,900 kila baada ya kipindi kitakachokubaliwa baina ya mkopaji na mkopeshaji.

Mtendaji mkuu huyo amesisitiza utatekelezwa kwa awamu kwenye nchi zote wanachama kwa shabaha ya kuhakikisha idadi ya wananchi wanaotumia huduma za TEHAMA kwenye ukanda huo inaongezeka.

Kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es salaam kimehudhuriwa na nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda Sudani Kusini na Burundi chini ya uratibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kikijadili hatua za ukuzaji sekta ya Mawasiliano katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa shabaha ya kusaidia ukuaji uchumi miongoni mwa wanachama wa Shirikisho hilo na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Washiriki wa mkutano huo wametaka kuwepo nia ya dhati kwa nchi wanachama katika kukuza chombo hicho ambacho wamesisitiza umuhimu wake katika kukuza sekta ya mawasiliano kwenye ukanda wa Afrika Mashariki haupaswi kutiliwa tashwishi.

Aidha washiriki wamebainisha mikakati itakayowezesha chombo hicho kuwa na mchango mkubwa katika sekta ya mawasiliano, sanjari na kuweka mpango mkakati utakaosaidia kupunguza vikwazo vya ukuaji wa chombo hicho katika kuharakisha ukuaji wa sekta ya Mawasiliano kwenye ukanda wa Afrika Mashariki.

Pia wamejadili namna wanavyoweza kukuza ujuzi kwa wanachama wao sambamba na kujadili namna watakavyodhibiti muingiliano wa mawasiliano ya simu hasa maeneo ya mpakani na kuona namna wanavyoweza kudhibiti changamoto hiyo katika maeneo husika.   

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mwenyekiti wa Shirikisho la Taasisi za TEHAMA Afrika Mashariki (EACO) akihitimisha mkutano huo alisisitiza umuhimu wa taasisi wanachama wa shirikisho hilo kuimarisha chombo hicho ili kiwe chenye manufaa zaidi katika sekta ya mawasiliano katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya alisisitiza kuwa suala la Mawasiliano linayo nafasi kubwa katika kukuza na kujenga Soko la Pamoja la Afrika mashariki.

Sudan Kusini yenyewe imebainisha kwamba EACO ni chombo muhimu kwa ukuaji wa sekta ya mawasiliano na kwamba chombo hicho kimekuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa sekta ya mawasiliano hasa mawasiliano ya simu.

Tanzania ni Mwenyekiti wa Shirikisho hilo ikitarajiwa kukabidhi uenyekiti kwa Rwanda baadae mwezi Julai mwaka huu.

Shirikisho la Mawasiliano la Afrika Mashariki (EACO) lilianzishwa mnamo 2012, kama taasisi inayojijitegemea kikanda likiwa na makao yake makuu mjini Kigali, Rwanda.

EACO huzileta pamoja Mamlaka za usimamizi wa Mawasiliano, watoa huduma (katika sekta ndogo za mawasiliano, utangazaji na posta), taasisi za mafunzo ya TEHAMA na wadau wengine katika sekta ya mawasiliano kutoka nchi za Burundi, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda lengo likiwa kuimarisha na kukuza ushirikiano katika usimamizi na matumizi ya sekta ya mawasiliano baina ya nchi sita za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika ukuzaji na utoaji wa huduma za posta, mawasiliano ya simu na utangazaji.

MWISHO.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!