JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Uwezeshaji wa Jamii za Afrika Kupitia Huduma za Posta


Uwezeshaji wa Jamii za Afrika Kupitia Huduma za Posta

Na Mwandishi Wetu, Arusha

WASIMAMIZI wa Sekta ya Posta Afrika pamoja na Mashirika ya Posta Afrika yanayo toa Huduma za Msingi wamekutana jijini Arusha jana, na kufanya mjadala juu ya: “Kubuni na Kubadili Mfumo wa Posta Afrika: Udhibiti, Ubunifu na Uwekezaji kwa Maendeleo Jumuishi ya Kijamii na Kiuchumi.”

Mkutano huo wa Viongozi wa juu ulioandaliwa na Umoja wa Posta Afrika (PAPU), ikiwa ni sehemu ya kikao cha 43 cha Baraza la Utawala la PAPU, Majadiliano hayo yalipelekea kugeuka kuwa jukwaa la kubadilishana ujuzi na uzoefu wa kitaaluma kupitia mijadala mbalimbali na wasilisho ikiwemo program tumizi: “Kuwezesha Jamii za Afrika Kupitia Huduma za Posta kuelekea Mapinduzi ya Pesa Mtandao kwa Haraka Barani Afrika – Kwa Simu Yoyote, Kazi Yoyote na Nchi Yoyote.”

Programu hiyo tumizi maalum  kupitia  simu janja inahusisha nchi zote 54 za Afrika kwa kuwezesha ununuzi wa bidhaa mbalimbali kwa kufanya malipo kidijitali moja kwa moja kutoka sarafu ya nchi moja kwendas sarafu ya nchi nyingine, kupitia teknolojia iliyoanzishwa na kampuni ya Uingereza iitwayo bibimoney. Kampuni ya Bibimoney inaongozwa Mkurugenzi Mtendaji bwana, Shiraz Jessa, aliezaliwa Jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Wasimamizi na Waendeshaji kutoka zaidi ya nchi 40 wanachama wa PAPU walitoa pongezi kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia – Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Jabiri K. Bakari, kwa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha shughuli za posta Afrika, ambapo Makao Makuu ya PAPU yanapatikana jijini Arusha.

Katika salamu zake za ukaribisho, Katibu Mkuu wa PAPU, Dkt. Chief Sifundo Moyo, alisifu mkutano huo akisema kuwa una umuhimu mkubwa kama jukwaa la kubadilishana uzoefu na kuhamasisha ukuaji wa maarifa. Akinukuu maneno ya Albert Einstein alisema: “Maarifa yanapatikana kupitia uzoefu.”

Alisema, kama mnavokumbuka, lengo kuu la mkutano huu ni kujenga jukwaa rasmi na la hadhi ya juu kwa ajili ya kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya Huduma za posta, hasa shughuli na usimamizi wa posta, pamoja na kuimarisha mtandao wa ushirikiano baina ya wadau wote.

Kwa upande mmoja, majadiliano ya kikao cha Wakurugenzi Wakuu wa Afrika yalibebwa na kaulimbiu isemayo: “Mustakabali wa Posta katika Ubunifu: Ujumuishi, Usafirishaji na Maendeleo Jumuishi ya Kijamii na Kiuchumi katika zama za Kidijiti.” Kaulimbiu hii imelenga kuleta hamasa kwa kuzingatia mazingira ya sasa ya mabadiliko ya haraka na teknolojia mpya zinazoibuka kila uchao, kupitia TEHAMA.

Tukio hilo lilikuwa fursa adhimu ya kutafakari namna ambavyo huduma za posta barani Afrika zinaweza kutumia kikamilifu teknolojia mpya kuelekea mustakabali wa bara letu pendwa kupitia huduma za posta za kidijitali, bunifu, jumuishi na zinazokidhi mahitaji halisi ya jamii.

Dkt. Moyo aliongeza kuwa, masuala yaliyowasilishwa na kujadiliwa yalilenga moja kwa moja katika muktadha wa kutimiza malengo yaliyowekwa na Ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2063 – Afrika Tunayoitaka, pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs).

Kwa upande mwingine, kaulimbiu ya jukwaa la 7 ilikuwa: “Changamoto za Kisheria, Kiufundi na Kifedha katika Kugharamia Huduma za Posta, na Mtazamo wa Baadaye.” Kaulimbiu hii ilikuwa muhimu kwa kuzingatia utafiti uliofanywa na Sekretarieti Kuu ambao ulionyesha kuwa asilimia 78 ya Nchi Wanachama haziwezi kugharamia mara kwa mara gharama za ziada zinazojitokeza katika utoaji wa huduma za posta kwa wote. Aidha, ni asilimia 7 tu ya Nchi Wanachama ndizo zimeweza kutekeleza mifumo ya kihasibu, ambayo ndiyo viwango vya juu vya kubaini gharama halisi ya huduma ya posta kwa wote.

Utafiti huo umekuwa fursa bora kwa wasimamizi na waendeshaji wa huduma za posta kutafuta suluhu za pamoja na zinazofaa ili kuzuia mgawanyiko wa huduma za posta na kuhakikisha huduma hizo zinaendelea kuwafikia watu wote, popote walipo katika nchi husika.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!