HUDUMA ZA INTANETI ZAPAISHA MAGEUZI YA KIDIJITALI

Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Tanzania yaendelea kupiga hatua kubwa katika mapinduzi ya kidijitali, huku idadi ya watumiaji wa intaneti ikifikia milioni 54.1 kufikia robo ya nne ya mwaka wa fedha 2024/2025, kwa mujibu wa takwimu kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Hili ni ongezeko kubwa kutoka milioni 29 mwaka 2020, hatua inayoakisi jitihada thabiti za serikali katika kuwekeza kwenye miundombinu ya mawasiliano na kuhimiza matumizi ya teknolojia ya habari nchini.
Kwa kipindi cha miaka minne, Tanzania imekuwa ikishuhudia ukuaji kwa watumiaji wa intaneti, unaochochewa na upanuzi wa huduma za mtandao kupitia simu za mkononi, kupungua kwa bei ya vifaa vya mawasiliano kama simu janja, pamoja na ongezeko la uelewa wa fursa za kidijitali miongoni mwa wananchi.
Hadi sasa, zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wanatumia huduma za intaneti — hatua inayoiweka nchi kwenye mkondo wa kujenga uchumi wa kidijitali wa kisasa na shindani.
Huduma za intaneti zimekuwa nguzo ya maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo biashara, elimu, afya, fedha, kilimo na utawala bora. Majukwaa ya kidijitali yamekuwa njia mpya na rahisi za kufanya biashara, kuwasiliana, kujifunza, na kupata huduma muhimu kwa ufanisi zaidi.
“Upatikanaji wa intaneti siyo tena anasa. Ni nyenzo muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Tumejipanga kuhakikisha kila Mtanzania, popote alipo, anaweza kunufaika na fursa za kidijitali.” Mkurugenzi Mkuu –TCRA Dkt. Jabiri Bakari
Maelfu ya vijana na wanawake wajasiriamali wanatumia mitandao ya kijamii na biashara mtandao kufanya biashara zao, kupata masoko mapya na kushiriki kwenye mnyororo wa thamani wa kidijitali.
Kupitia TCRA, serikali imeweka mazingira bora ya ukuaji wa teknolojia kwa kuanzisha programu mbalimbali za kuhamasisha ukuaji wa TEHAMA hasa kwa kundi la vijana waliomo mashuleni kama vile klabu za kidijitali, wasichana katika TEHAMA, na mashindano ya Cyber Champions ambayo yanajenga uelewa na ujuzi wa teknolojia miongoni mwa vijana.
Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya wanawake, vijana, na wananchi wa vijijini wanaopata huduma za mtandao inaendelea kuongezeka, kutokana na juhudi za serikali kupitia TCRA kuhamasisha uwekezaji kwenye eneo la Mawasiliano.
“hivi karibuni tumeendesha mnada wa Masafa ambao makampuni yaliyoshiriki na kushinda yanaenda kuongeza wigo wa huduma zao hasa maeneo ya pembezoni na kuimarisha huduma za masafa ya 5G” Mkurugenzi Mkuu –TCRA Dkt. Jabiri Bakari
Tanzania sasa inaingia rasmi katika zama za uchumi wa kidijitali. Ukuaji huu wa haraka unasukumwa na teknolojia ya 5G, upanuzi wa vituo vya kuhifadhi data (data centres), matumizi ya kompyuta za wingu (cloud computing), na huduma za serikali kwa njia ya mtandao zinazorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
TCRA imesisitiza kuwa ukuaji huu lazima uende sambamba na uwekezaji katika usalama wa mtandao, ulinzi wa taarifa binafsi, na elimu ya matumizi salama ya teknolojia kwa umma.