KAMPENI YA “FUTA DELETE KABISA” YAZINDULIWA KUTOKOMEZA UPOTOSHAJI MTANDAONI!

Na mwandishi wetu - Dodoma
WANANCHI wameshauriwa kujilinda na taarifa Potofu, Uzushi, Uhalifu na Ulaghai mtandaoni kwa Kuongeza Umakini na Kufuta Kabisa taarifa hizo Feki wanapotumia mtanddo. KATIKA jitihada za kukabiliana na ongezeko la taarifa za upotoshaji mtandaoni, TCRA imezindua kampeni kabambe yenye kauli mbiu "Futa Delete Kabisa".
Akizungumza na gazeti hili, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusuiano kwa Umma – TCRA Bw. Rolf Kibaja alieleza jijini Dodoma jana, kuwa kampeni hii inalenga kutoa elimu kwa umma kuhusu usalama wa taarifa pamoja na umuhimu wa kuhakiki taarifa zinazopokelewa kabla ya kusambaza .Kibaja alieleza kuwa jamii imekumbwa na wimbi la taarifa zakizushi mtandaoni, hasa taarifa zisizo rasmi zinazoweza kuchochea taharuki na kuvuruga amani.
Ameongeza kuwa kampeni ya "Futa Delete Kabisa" inamuwezesha mwananchi kuepuka madhara ya kisheria yanayotokana na kusambaza taarifa potofu. “Kupitia kampeni hii, wananchi watajifunza namna ya kutambua taarifa zenye viashiria vya uchochezi na jinsi ya kuchukua hatua stahiki” amesema Bw. Rolf Kibaja.
Kwa upande mwingine, Kibaja aliongeza kuwa kwa sasa kuna wimbi la taarifa za uzushi zinazozatengenezwa kwa kutumia akili unde (AI). Katika kukabiliana na hilo TCRA imetoa wito kwa jamii kuhakiki uhalisia wa taarifa kabla ya kusambaza. “Unaweza kutumia teknolojia saidizi (reverse image searching) kubaini uhalisia wa taarifa ya picha ikiwemo uchapaji wake wa mara ya kwanza au kwa kuangalia viashiria kama vile takwimu zisizo sahihi, makosa ya kisarufi au majina na kuwa vihisishi vingi vyenye kuongeza chumvi” Bw. Rolf Kibaja
Afisa Mhifadhi Mwandamizi wa TCRA, Bw. Raphael Mwango, alisisitiza kuwa kizazi cha sasa kinafikiwa na taarifa kwa haraka tofauti na zamani. Ameeleza kwamba vijana wengi huanza kutumia simu janja mapema, hali inayowapa fursa ya kupata taarifa mbalimbali – nzuri na potofu.
Bw. Mwango amesema kampeni hii ni jibu la kimkakati kukabiliana na changamoto za taarifa potofu, huku ikilenga kuwasaidia vijana na wazazi kujilinda kisheria. Ameeleza pia kuwa uzushi unaweza kuathiri afya ya akili, kuvruga mshikamano wa wananchi, kuharibu heshima ya mtu au hata kuchangia vifo, jambo linaloipa kampeni hii uzito wa kipekee.
Mwango amesema kampeni ya "Futa Delete Kabisa" itatekelezwa kwa muda wa miezi sita na kuongeza kuwa TCRA imejipanga kukabiliana na changamoto hii kwa kuwahamasisha wananchi kutumia teknolojia kwa uangalifu na kufuata taratibu zilizo sahihi.
Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu, Kibaja alitoa wito kwa wananchi kuwa makini na taarifa wanazopokea au kusambaza mtandaoni. Alisisitiza kuwa taarifa kuhusu matokeo ya uchaguzi zisizotolewa rasmi zinaweza kusababisha migogoro na taharuki isiyo ya lazima.
Aidha wananchi wameshauriwa kutumia namba 15040 kuripoti namba za matapeli kwa ujumbe mfupi, na *106# kuhakiki taarifa zao, huku namba 100 ikiwa ndiyo rasmi ya watoa huduma. Kwa ujumla, "Futa Delete Kabisa" si tu kampeni ya elimu, bali ni mwamko mpya wa kulinda amani, usalama na utu wa jamii ya Kitanzania.