Maboresho ya Sera na Makerebisho ya Muundo wa Usimamizi vyapaisha Huduma za Kiposta

Na Mwandishi Wetu
MAKALA hii imejikita kwenye maboresho na mipango inayotelekezwa kwenye Sekta ya Posta Tanzania na inayolenga kuendeleza utoaji huduma kwa ufanisi na usalama zaidi.
Tanzania imefanya maboresho makubwa kwa kuanzisha mipango ya kuendeleza uvumbuzi, kujenga miundombinu inayowezesha kupaisha huduma mpya na kusimamia hatua za kuhakikisha usalama wa huduma kwenye sekta ya Posta.
Maboresho na Mageuzi haya yanatokana na mahitaji ya soko na pia yamezingatia mwelekeo wa matumizi na mahitaji ya watumiaji. Vilevile yametokana na umuhimu wa kuleta ufanisi kwenye sekta ya huduma za Kiposta ili kuifanya ishindane kwenye utoaji wa huduma za mawasiliano, ndani nan je ya Nchi.
Kipaumbele kikubwa ni kuzifanya huduma za Posta kuwa za kidijiti. Hii inatokana na mahitaji na matarajio ya uchumi wa kidijitali.
Uchumi wa Kidijitali ni ule ambapo nchi inajenga mwelekeo tawala wa matumizi ya Uchumi wa Kidijitali ni ule ambapo nchi inajenga mwelekeo tawala wa matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) na mifumo ya kielektroniki kwenye sekta zote.
Watoa huduma za Posta na usafirishaji vifurushi duniani kote wanazidi kutumia teknolojia mpya kuboresha huduma zao na kuanzisha maeneo mapya ya biashara. Hii inatokana na matarajio ya watumiaji na mahitaji ya soko, ambalo limehama kutoka barua za kawaida kwenda kwenye vifurushi na vipeto vinavyo simamiwa na kufuatiliwa kwa mifumo ya kielektroniki, kwamfano huduma ya Posta Kiganjani.
TEHAMA za kisasa na program tumizi zinazotokana nazo na matumizi yake kwenye mlolongo mzima wa utoaji huduma za posta na usafirishaji vifurushi zimeleta fursa mpya kwa watoa huduma kuanzisha aina mpya ya shughuli na huduma.
Wanatumia kikamilifu fursa zionazowezesha biashara mtandao, ambayo inawawezesha watumiaji kununua na kuuza bidhaa mtandaoni na kuzifikisha au kuzichukua kwa wateja kwenye ofisi na makazi yao.
Huduma za Posta na Usafirishaji vifurushi zinachangia kwa kiasi kikubwa kwenye ajenda ya maendeleo ya Tanzania. Mipango ya Kisera na mifumo ya kiusimamizi nchini imezingatia viashirio wezeshi vya biashara mtandao.
Kukua kwa mawasiliano ya simu za mkononi, matumizi ya intaneti, mitandao ya kijamii, fursa za masoko na urahisi wa kufanya miamala vimesukuma biashara mtandao Tanzania.
Tanzania ina miundombinu muhimu na program tumizi za kuwezesha huduma za intaneti ya kasi. Aidha, ina mfumo imara wa malipo.
Taarifa robo mwaka, ilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri K. Bakari imeainisha kwamba hadi Juni mwaka huu, kulikuwa na watumiaji wa intaneti 54,078,530 na akaunti za pesa kwa simu 68,059,290. Hivi vyote ni vya msingi ili kuwezesha, kufanikisha na kuendeleza biashara mtandao, zikiwemo za Kiposta.
Tanzania imepanua miundombinu inayowezesha jamii zilizoko maeneo ya pembezoni kupanua fursa zake kiuchumi, kwa kutumia mifumo inayowezeshwa kidijiti.
Nchi hii imepanua kuenea kwa teknolojia ya uzao wa tatu (3G), wa nne (4G) na wa tano (5G) wa teknolojia za mawasiliano ya mkononi.
Taarifa ya sasa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dr Jabiri iembainisha kwamba Uzao wa Tatu umeenea miongoni mwa watu asilimia 93.4 ya watu, kutoka 89 na Uzao wa Nne asilimia 92 kutoka 83 kwakipindi kutoka Aprili hadi Juni 2025. Kuenea 3G kijiografia ni asilimia 75, kutoka 73 na 4G asilimia 75, kutoka 69.
Uzao wa Tano (5G) umeenea kwa kwa asilimia 5.9 Juni 2025 kutoka asilimia 2 Juni mwaka jana. Ulienea kwa asilimia 3.6 ya watu Machi mwaka huu. Teknolojia hiyo imefika asilimia 26 ya eneo la Tanzania, kutoka asilimia 15 Juni 2024 na 23 Machi mwaka huu. Ilienea kwa asilimia 5.9 miongoni kwa watu Juni 2025 kutoka asilimia 2 Juni mwaka jana.
Kuenea huku kumewezesha Watanzania wengi zaidi kutumia huduma za intaneti. Teknolojia mpya zinawezesha watumiaji kutumia data popote walipo. Bidhaa na huduma zinaweza kununuliwa mitandaoni kutoka maeneo ya pembezoni na vijijini.
Watoa huduma pia wanatumia vifaa vya mkononi, vinavyoitwa PDA kutuma taarifa za vifurushi na vipeto kutoka maeneo mbalimbali kwenye mifumo yao ya data na kumbukumbu.
Tanzania pia inatekeleza mpango wa kutoa anwani za makazi ya watu popote walipo. Mfumo wa anwani za makazi na postikodi (NAPS) unatoa anwani maalum ya kudumu na inayoweza kuhakikiwa.
Hii inafanikisha ufikishaji na uchukuaji wa vitu vinavyotumwa kwa Posta, inaongeza ufanisi na inajenga imani ya watumiaji kwa huduma za Posta na usafirishaji vifurushi. Vilevile inafanya huduma za posta kutegemewa zaidi.
Kabla ya NAPS ufanisi wa kufikisha na kuchukua vifaa vya posta ulitegemea maelezo ya namna ya kufika eneo kwa kufuata maelezo marefu. Wahusika walielekezwa kufika maeneo husika kwa kuona vitu na majengo makubwa. Uelekezaji huu usiokuwa rasmi ulichelewesha huduma, kupotea vitu vya posta na watoa huduma au wakala wao kushindwa kuvifikisha au kuvichukua.
Mfumo wa NAPS umeunganishwa na mifumo ya taasisi 18 ya ufikishaji vitu. Hizi ni pamoja na Shirika la Posta Tanzania (TPC) na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).
TTCL inatoa huduma za kufungia watu intaneti ya kasi ya waya za faiba ofisini, sehemu za biashara na kwenye makazi.
Pamoja na kufanikisha uchukuaji na ufikishaji wa vitu kwa mtumaji au mpokeaji pale alipo, mfumo wa NAPS unawezesha serikali na wakala wake kutekeleza mipango yake kama inavyokusudia, ikiwemio kuwasiliana na wananchi kwa ufanisi.
Mfumo unaendeleza usalama, ulinzi wa watu na mipango ya huduma mbalimbali. Unawezesha huduma za dharura kama vile ambulensi, polisi na zimamoto na uokoaji. Pia unawezesha mipango miji na ufikishaji wa huduma za uchumi na jamii kwa ufanisi.
Kufikia Machi 2025, anwani zaidi ya milioni 12.8 zilikuwa zimesajiliwa kwenye NAPS.
Kanuni za Posta zilirekebishwa mwaka 2024 ambako ulianzishwa mfumo wa matumizi ya postikodi kibiashara. Kanuni zimeweka aina tano za postikodi. Hizi ni za maeneo ya biashara na kazi, watumiaji wakubwa wa huduma za posta na usafirishaji vifurushi, ofisi za posta, vitu na maeneo muhimu na za muda kwa ajili ya matukio na shughuli mbalimbali.
Kwa mfano mtu akiwa na shughuli inayohitaji watu wafike bila bughudha, anaomba na kupewa postikodi ya muda ambayo atawatumia wadau wake ili waweze kufika kwa urahisi.
Mtoa huduma za posta kitaifa – TPC – ameanzisha biashara na shughuli kwenye maeneo mengine. Anatumia uvumbuzi na ubunifu kwenye shughuli zake ili kuleta ufanisi, uwazi na kuridhisha wateja wake.
TPC inatekeleza mipango ya kidijitali kuwezesha huduma za posta kwenye maeneo muhimu. Mifumo ya kidjitali inatumika kwenye kuweka kumbukumbu za mapato, kufuatilia vitu kwa wakati na kuboresha uchukuaji na uwasilishaji wa vitu vya posta. Vilevile inawezesha uzingatiaji wa viwango vya huduma.
Tanzania inatelekeza mipango kuhakikisha uimara na usalama wa mitandao yake ya mawasiliano. Kwenye sekta ya posta hatua ni pamoja na kulinda wafanyakazi, mali na vifaa vinavyopita Posta. Usalama umeimarishwa kwenye mlolongo wote wa utoaji huduma za posta. Kanuni za posta zimeweka miongozi kuhusu vitu visivyotakiwa kusafirisha kwa kwa posta au vinavyothibitiwa ili kuhakikisha usalama na uimara wa mifumo.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Jabiri alisema jijini Dar Es salaam hivi karibuni kwamba, utafiti uliofanywa na Shirika la Mwasiliano Ulimwenguni (ITU)-Geneva, kuhusu Uthabiti wa Mifumo ya mtandao “Tanzania ni ya Kwanza Afrika Mashariki, ya Tatu Afrika na ni miongoni mwa nchi 46 zinazoongoza duniani kwa Ufanisi kwenye mifumo ya Usalama Mitandaoni”.
Tanzania imepewa nafasi ya juu na ni miongoni kwa nchi mifano kutokana na utekelezaji wa mipango mbalimbali kwenye maeneo matano ya yanayoonesha umakini kwenye usimamizi wa usalama mtandaoni.
Maeneo hayo ni hatua za kisheria, kiufundi, kimfumo, kuendeleza utendaji na ushirikiano kimataifa.
Hatua za kisheria yanahusisha sheria na kanuni zinazosimamia usalama mitandaoni na njia ya kukabiliana na uhalifu mitandaoni. Tanzania ni mojawapo ya nchi zenye sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi.
Usalama mitandaoni ni suala mtambuka. Unahusisha sekta zote zikiwepo za Kiposta. Serikali inatekeleza mpango maalum wa wa elimu na kuongezwa uelewa watu kuhusu Usalama Mitandaoni.