Madereva Bodaboda na Wajasiriamali Wanawake wapewa Elimu ya Usalama Mtandaoni

Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imefanya mafunzo ya usalama mtandaoni na manufaa ya TEHAMA kwa umoja wa wanawake wajasiriamali na madereva Bodaboda.
Akizungumza na washiriki wa semina hiyo ambayo ni kuelekea maadhimisho ya siku ya usalama mtandaoni Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA Dkt. Jabiri Bakari amesema,elimu endelevu ya usalama mtandaoni ni muhimu ili kufanya teknolojia iwe na tija kwa wananchi. Dkt Bakari amesema mtandaoni fursa ya wajasiriamali kuwafikia wateja wao.
“Bodaboda anayetumia TEHAMA anawafikia wateja wengi zaidi kuliko yule asiyetumia fursa hiyo na Mamantilie atumiaye mifumo hii anawasiliana na wateja wake kwa urahisi zaidi ” alisisitiza Dkt. Bakari.
Innocent Ndowo kutoka jeshi la polisi kitengo cha uchunguzi wa makosa ya mtandaoni katika wasilisho lake amewasisitiza wajasiramali, madereva Bodaboda na jamii kwa ujumla kuripoti Polisi pindi wanapofanyiwa uhalifu mtandaoni.
Mafunzo hayo yameshirikisha jeshi la polisi, Umoja wa watoa huduma za simu (TAMNOA) na Benki (Huduma za mtandaoni) ambapo mada zilizowasilishwa zimegusa masuala ya elimu ya namna bora ya kufanya biashara na kuwa salama mtandaoni.
Siku ya usalama mtandaoni (Safer Internet Day) ambayo ni mpango wa kimataifa ulioanzishwa mwaka 2004 kwa lengo la kuhamasisha matumizi sahihi na salama ya mtandao wa intaneti hufanyika kila jumanne ya pili ya mwezi Februari kila mwaka ambapo mwaka huu itakuwa Februari 6.