JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Mpango wa Unafuu wa Gharama za Simu EAC Wazaa Matunda


Mpango wa Unafuu wa Gharama za Simu EAC Wazaa Matunda

Na mwandishi wetu

GHARAMA za maongezi kwa simu kutoka Tanzania kwenda nchi nyingine Afrika Mashariki zilishuka kwa asilimia 61 kati ya Aprili na Juni 2025 kufuatia utekelezaji wa makubaliano ya pamoja kupunguza gharama za simu kwa watumiaji wanaotembelea mojawapo ya nchi hizo, taarifa zimethibitisha.

Ripoti ya hali ya mawasiliano Tanzania katika robo mwaka ya Aprili hadi Juni mwaka huu inaonesha kuwa wastani wa gharama za siku kwenda nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zilipungua kutola shilingi 627.80 kwa dakika Machi hadi 247.52 Juni mwaka huu.

Ripoti hiyo, iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt Jabiri Bakari inaeleza kuwa dakika za maongezi ya simu kutoka Tanzania kwenda nchi nyingine EAC zimeongezeka kutoka 9,097,165 robo mwaka ya Aprili-Juni 2021 hadi 156,913,941 Aprili-Juni 2025.

Kwa simu za humu nchini, wastani wa bei za kupiga simu (bila kifurushi) haujabadilika tangu Juni mwaka jana. Umebakia shilingi 26 kwa simu kwenye mtandao wa mtumiaji (on-net) na shilingi 28 kwenda mtandao mwingine (off-net).

Meseji (SMS) za ndani zinatozwa shilingi 7.80 na za kwenda nje shilingi 189.60 kwenye mitandao yote. Bei za data zimebakia shilingi 9.35 kwa megabaiti (MB).  

MB ni kipimo cha ukubwa wa data kwenye matumizi ya kompyuta, ambamo kila herufi, namba, alama ni baiti moja. Zikiwa 100 ni kilobaiti (KB) na elfu ni megabaiti (MB).

Uchambuzi wa ripoti ya TCRA unabainisha kuwa wastani wa gharama za kupiga simu unatokana na gharama ndogo za mtoa huduma mmoja anayetoza chini ya wastani kwa kiasi kikubwa. Halotel wanatoza shilingi 10 kwa maongezi kwenye mtandao wao, shilingi 20 kwenda mitandao mingine na shilingi tano (5) kwa SMS.

 Airtel, Yas, TTCL na Vodacom wanatoza shilingi 30 kwa maongezi ndani na nje ya mitandao na shilingi nane (8) kwa meseji.

Gharama za kupiga simu bila kifurushi zilipungua kwa asilimia 21 kati ya Juni 2021 na Juni mwaka huu – kutoka shilingi 34 kwa dakika ndani na nje ya mitandao. Bei za SMS za ndani zimepungua kwa asilimia 67 – kutoka shilingi 13 hadi zinazotozwa sasa.

Kwa upande wa vifurushi, gharama za simu ndani ya mtandao zimebakia shilingi 4.80 tangu Septemba 2024 wakati nje ya mtandao zimeshuka kutoka shilingi 6.07 kwa dakika machi 2025 hadi 5.96 Juni mwaka huu. Vifurushi vya data vinatozwa shilingi 2.12 kwa MB na SMS za ndani shilingi 2.12.

Gharama za vifurushi vya maongezi zilishuka kwa asilimia 71 kati ya Juni 2021 na Juni mwaka huu – kutoka  wastani shilingi 8.3 kwa dakika kwenye mitandaoi yote hadi zinazotozwa sasa. Bei za vifurushi vya data zilikuwa shilingi 1.61 kwa MB mwaka 2021, zikaongezeka hadi 2.17 na kubakia 2.12 kuanzia Machi mwaka huu.  

Ripoti inasema wateja wa mitandao ya simu za mkkononi walitumia dakika bilioni 43.3 kwenmye robi mwaka ya Aprili hadi Juni mwaka huu, kutoka bilioni 40.6 billion robo mwaka iliyoishia Machi mwaka huu.

Wakati huo huo, simu zenye uwezo mkubwa, maarufu kama simu janja, zimeenea kwa asilimia 37 miongoni mwa watu. Hii inawezesha watumiaji wengi kutumia huduma zinazotokana na teknolojia za kisasa na za uzao wa mbele wa mawasiliano kupitia vifaa vya mkononi.

Taarifa hiyo imesema ueneaji wa teknolojia za uzao wa tatu (3G) na wa nne (4G) uliongezeka kwa kati ya asilimia 11 na tano kati ya Juni 2024 na Juni mwaka huu. Kuenea kijiografia nchini kuliongezeka kwa asilimia 8.7 katiya  Juni 2024 na Juni 2025.

Uzao wa tatu umeenea miongoni mwa watu asilimia 93.4 ya watu, kutoka 89 na uzao wa nne asilimia 92 kutoka 83 kipindi hicho. Kuenea 3G kijiografia ni   asilimia 75, kutoka 73 na 4G asilimia 75, kutoka 69. 

Uzao wa 5G ulienea kwa kwa asilimia 5.9 miongoni kwa watu kufikia Juni 2025 kutoka asilimia 2 Juni mwaka jana na asilimia 3.6 ya watu Machi mwaka huu.  Teknolojia hiyo imefika asilimia 26 ya eneo la Tanzania, kutoka asilimia 15 Juni 2024 na 23 Machi mwaka huu.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!