JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Nnauye Ataja Mikakati Kuondoa Mapengo ya Upatikanaji Mawasiliano


Nnauye Ataja Mikakati Kuondoa Mapengo ya Upatikanaji Mawasil...

Tanzania imeanzisha mipango ya kuwezesha wananchi wake kufaidi kikamilifu fursa zi tokanazo na teknolojia ya habari na Mawasiliano (TEHAMA) kama sehemu ya mikakati ya kueneza huduma za mawasiliano kwa wote, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye amesema.

Katika ujumbe wake Siku ya Mawasiliano Afrika tarehe 7 Desemba mwaka huu, Mhe. Nnauye amesema Serikali itahakikisha kwamba Watanzania wote wanakuwa na stadi muhimu za kuwawezesha kutumia huduma za kidijitali.

Stadi za kidijitali ni muhimu kuhakikisha Wanzania wanajumuika katika mifumo ya kidijitali, amesema.

 “ Serikali inawekeza kwenye mipango ya kuwawezesha wananchi kupata stadi muhimu za kutumia mifumo ya kidijitali. Tunatekeleza mipango kuelekea kuhakikisha kwamba  kila Mtanzania, bila kujali hali yake, anatakiwa kupata stadi muhimu za kidijitali kumuwezesha kuendesha maisha yake kwenye dunia ya kidijitali”, amedokeza.

Mikakati hiyo  inahusu kushughulikia tofauti zilizopo katika kuenea kwa miundombinu, hoja kuhusiana na watumiaji kutomudu gharama na kutoa elimu ya masuala ya kidijitali inayolenga kuwezesha jamii mbalimbali, Mhe. Nnauye ameongeza.

Waziri Nnauye amesema Serikali ingependa kuhakikisha usalama na faragha za watu wote na kutekeleza mipango ya kuwakinga dhidi ya tishio la matumizi mabaya ya mitandao na pia kulinda miundombinu ya kidijitali ya nchi ili kuhakikisha uimara wake.

Tarehe 7 Desemba kila mwaka ni siku ya kumbukumbu ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mawasiliano ya Simu Afrika (ATU)  mwaka 1977 kama chombo mahsusi cha Umoja wa Afrika kinachoshughulikia TEHAMA. Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni: Kuelekea Mabadiliko ya Kidijitali ya Kujumuisha walioachwa na walio pembeni: Kushughulikia Masuala ya Upatikanaji kwa matumizi.

“ Ujumuishaji wa kweli kidijitali unategemea upatikanaji kwa matumizi. Sera zetu na mipango yetu vimejikita kwenye msingi kwamba teknolojia ipatikane kwa wote kwa ajili ya matumizi, ikiwa ni pamoja na wale wenye vikwazo vinavyotokana na hali yao, uchumi, au vya kijamii”, Mhe. Waziri ameeleza.

Katika ujumbe wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabiri Kuwe Bakari amesema Mamlaka imeanzisha mipango maalum kuhakikisha kwamba jamii za pembazeni na zilizoachwa zinaunganishwa.

Amefafanua kwamba TCRA inaongoza utekelezaji wa mipango ya kufanikisha ruzuku kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu maeneo ya vijijini ili kuhakikisha huduma za mawasiliano ya simu ambazo wengi watamudu gharama zake zinapatikana na kutumiwa.

TCRA inaweka mazingira wezeshi ya kiusimamizi, inahimiza mipango inayolenga kueneza huduma na inashirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kwamba matunda ya mabadiliko ya kidijitali yanasambazwa kwa usawa pote, hasa kuzifikia jamii za Watanzania walio pembeni na jamii zilizoachwa, Dkt. Jabiri ameongeza.

Mipango hiyo ni pamoja na kuendeleza klabu za kidijitali kwenye shule na vyuo ili kupanua uelewa wa masuala ya TEHAMA na uchumi wa kidijitali, na pia kuanzisha fursa za kujenga stadi za TEHAMA, Mkurugenzi Mkuu amesema.

“ Kwa kuwezesha jamii kuanzia umri mdogo kwa kuzipatia stadi za kidijitali zinazohitajika, TCRA inachangia kuwezesha kufikiwa lengo la kuendeleza jamii inayotumia mifumo ya kidijitali, na inaonesha elimu ya masuala ya kidijitali ina nguvu kubadili na kushirikisha jamii, amefafanua.

TCRA pia inaendelea mpango wa kuinua wabunifu kwenye sekta ya TEHAMA, kwa kuwapatia bila malipo na kwa vipindi maalum, raslimali adimu za mawasiliano kama vile namba na masafa ya mawasiliano, ili wajaribishe uvumbuzi wao na miradi yao. Mpango huu unatekelezwa kwa pamoja na Tume ya Tanzania ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).

Katibu Mkuu wa ATU, Bwana John Omo amesisitiza umuhimu wa kushughulikia tofauti za upatikanaji na matumizi ya intaneti ambazo zinasababishwa, pamoja na mambo mengine, na hali za kijiografia, viwango vya mapato na jinsia. Ripoti mbalimbali zinaonesha kwamba matumizi ya intaneti ni kidogo vijijini na miongoni mwa wanawake kulinganisha na mijini na matumizi kwa wanaume.

Bwana Omo amedokeza kwamba asilimia 72 ya watu Afrika hawapati huduma za intaneti kupitia vifaa vya mkononi, na kwamba karibu watu milioni 200 Barani humu wanaishi kwenye maeneo ambayo hayana mitandao ya intaneti ya kasi.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!