JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

TCRA: ‘Wasafirishaji Vifurushi na Vipeto Hakikisheni Mnazo Leseni’


TCRA: ‘Wasafirishaji Vifurushi na Vipeto Hakikisheni Mnazo L...

 

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka watoa huduma za usafirishaji wa vifurushi na vipeto ambao hawana leseni za kutoa huduma husika, kujiandikisha mara moja kwa njia ya Mtandao na kupata leseni kutoka mamlaka hiyo.

Akizungumza jijini Dar es salaam jana Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dk. Jabiri Bakari, alisisitiza kuwa TCRA imezindua kampeni ya Elimu kwa Umma ili kuwahamasisha Watoa Huduma za Usafirishaji kuhakikisha wanarasmisha huduma zao ili kuongeza wigo wa haki na wajibu kwao na wananchi wanaowahudumia.

Alieleza kuwa utoaji wa leseni kwa watoa huduma za usafirishaji wa vifurushi na vipeto ambazo ni huduma za kiposta huimarisha uwajibikaji wao kwa wananchi wanaowahudumia.

"Kama Mamlaka inayohusika na sekta, tunatambua jukumu muhimu wanalolitekeleza katika kusaidia shughuli za kiuchumi. Ni jukumu letu kuwakumbusha watoa huduma za usafirishaji vifurushi na vipeto kujisajili na hatimae kupata leseni ya TCRA," alisisitiza Dk. Bakari.

Dk. Bakari alisema kuwa kampeni hiyo inalenga kutatua changamoto zinazokabili watumiaji wa huduma za usafirishaji wa vipeto na vifurushi.

Aliwaasa watumiaji wa huduma za usafirishaji vifurushi na vipeto kutumia huduma za wasafirishaji waliothibitishwa na wenye leseni, ambao wana ofisi, vituo vya kuhifadhia mizigo, rekodi nzuri ya ufanisi, usalama, na uadilifu katika utoaji wa huduma hizo, ambao TCRA huwakagua kujiridhisha na Kiwango cha ubora wa huduma wanazotoa.

"Kufanya biashara ya huduma za usafirishaji vipeto na vifurushi bila kuwa na leseni inayotolewa na TCRA ni kinyume na taratibu za kisheria zilizowekwa," alisema, akiongeza kuwa wale wanaohitaji kusajili shughuli hizo wanaweza kuwasilisha maombi yao mtandaoni kupitia portal maalum inayopatikana kupitia www.tanzaniteportal.go.tz ambapo watawasilisha maombi na kupatiwa leseni kwa wakati.

"Tumefanya maboresho makubwa katika huduma zetu, na waombaji wote wa leseni za Mawasiliano wakiwemo wanaohitaji kutoa huduma hizi za usafirishaji vifurushi na vipeto sasa wanaweza kupata leseni zao kupitia mfumo wetu wa kuwahudumia wateja ambao unapatikana kupitia tovuti ya Tanzanite," alisisitiza.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliyopewa wajibu wa kusimamia Mawasiliano nchini hutekeleza jukumu hilo kwa kusimamia Makundi matatu ya sekta hiyo ambayo ni mawasiliano ya simu na intaneti, huduma za Posta na Utangazaji, katika usimamizi wa sekta ya posta Mamlaka hiyo hutoa leseni na kusimamia masharti ya leseni kwa watoa huduma za usafirishaji wa vifurushi na vipeto leseni zilizoganywa katika Makundi sita yaani watoa huduma za usafirishaji vifurushi na vipeto wa kimataifa, Afrika Mashariki, ndani ya mji mmoja na kati ya miji.

MWISHO

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!