Wanafunzi wabuni Mfumo wa kuwezesha malipo ya umeme moja kwa moja kuingia kwenye mita
Na mwandishi wetu,
Wanafunzi kutoka shule za Zanzibar wamebuni mfumo unaowezesha malipo ya umeme kuingia moja kwa moja kwenye mita bila mnunuzi kulazimika kuingiza mita namba za umeme. Wakionyesha jinsi mfumo huo unavyofanya kazi kwenye Maonyesho ya maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Wasichana na TEHAMA yaliyofanyika tarehe 25/04/2024 jijini Arusha, wanafunzi hao wamesema mfumo huo utasaidia kurahisisha huduma za umeme kwa watumiaji na kuboresha huduma zinazotolewa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Akielezea suluhisho hilo Mwanafunzi Salina Sharif kutoka Zanzibar amesema walibuni mfumo huo kutokana na kuona tatizo la wananchi kushindwa kuunganisha umeme kwa njia ya mtandao. Mfumo huo walioupa jina la Power Pals unatoa suluhisho ya mtumiaji wa umeme kuingiza namba za umeme bila kulazimika kuweka namba hizo kwenye mita ya umeme. “Power Pals inakusuhulishia kutia umeme mtandaoni bila ya kwenda nje kujitafutia matatizo”
Akitoa maelezo ya ziada kuhusu mfumo huo Bi Salina Sharif amesema ili kutumia mfumo huo, mtumiaji atapaswa kuwa ameshaunganishiwa na huduma ya umeme, kifaa cha mita ya kuingiza umeme pamoja na kuunganishwa na mfumo wa malipo mtandaoni kwa njia ya simu.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Jabiri Bakari alisema kuwa Mamlaka ya Mawasiliano kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) inaunga mkono kazi za ubunifu wa kiteknolojia kwa kutoa rasilimali za mawasiliano zinazohitajika bure kwa kipindi cha miezi mitatu ili kuwawezesha na kuinua bunifu zao. Amesema miaka ya nyuma ilikuwa ngumu kwa wabunifu kufanya tafiti ya bunifu zao za kiteknolojia kwa kuwa walikuwa wanalazimika kununua rasilimali za mawasiliano kama Masafa lakini kwa sasa TCRA inawezesha kutoa rasilimali hizo bila gharama yoyote kwa kipindi cha siku tisini.
Ameongeza kuwa COSTECH wana mchango katika kutambua iwapo wazo hilo la kiubunifu litaleta manufaa kwa jamii endapo litapatiwa rasilimali hizo na kuendelezwa kwaajili ya kutumia teknolojia katika kutatua changamoto mbalimbali. Aidha, wanatoa mwongozo ya utaratibu mzuri utakaofuatwa ili wanafunzi na wabunfiu wengine waweze kunufaika na kujiendeleza kimaisha. Dkt. Jabiri amewasihi wabunifu mbalimbali kutumia fursa hiyo kikamilifu ili kuchochea maendeleo ya teknolojia yatakayosaidia kukuza uchumi wa kidigiti.
Wanafunzi hao walioshiriki kwenye maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Wasichana na Teha
Maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Wasichana na TEHAMA huadhimishwa kila Alhamisi ya mwisho wa Mwezi wa Aprili kwa lengo la kuhamasisha wasichana kuchukua masomo ya sayansi. Siku hiyo inatokana na makubaliano ya nchi wanachama wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya TEHAMA (International Telecommunications Union - ITU). Kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka 2024 ni “Uongozi”