JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Tanzania Yachagiza Mabadiliko ya Sekta ya Posta Afrika


Tanzania Yachagiza Mabadiliko ya Sekta ya Posta Afrika

Na Mwandishi Wetu – ARUSHA

SERIKALI ya Tanzania imezihimiza Nchi Wanachama wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU) kujenga mazingira ya mabadiliko yatakayoiwezesha sekta hiyo kuendelea kuwepo na kutimiza matarajio ya wateja wa huduma za posta.

Akifungua Mkutano wa 43 wa Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Afrika (PAPU) uliofanyika jijini Arusha jana, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Nicholaus Merinyo Mkapa alisema utoaji wa huduma za sekta ya posta unapaswa kuendana na mabadiliko ya haraka ya mahitaji na matarajio ya wananchi, akisisitiza kuwa Tanzania imejizatiti kuyafikia malengo hayo.

“Napenda kuthibitisha tena dhamira thabiti ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuunga mkono shughuli za Umoja wa Posta Afrika. Uwepo wenu hapa leo ni kielelezo cha dhamira yetu ya pamoja ya kuimarisha mazingira ya posta na mawasiliano barani Afrika kwa manufaa ya wananchi wetu,” alisema.

Katika hotuba yake ya ufunguzi aliyoitoa katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabiri K. Bakari aliwahimiza wanachama wa PAPU kutumia mifumo ya kidijitali kuleta ustawi wa sekta ya posta Afrika ili kuleta maendeleo endelevu na kuboresha maisha ya watu.

Katika hotuba hiyo kwa niaba yake, Meneja wa Huduma za Posta TCRA, Bi. Cecilia Mkoba, Mkurugenzi Mkuu Dkt. Jabiri  alisema kuwa kanuni za Usimamizi wa sekta ya posta hazipaswi kuwa kikwazo, bali ni kichocheo cha kuwawezesha wananchi kupata huduma mbalimbali.

“Tunapaswa kutambua kuwa usimamizi si kizuizi, bali ni daraja. Usimamizi madhubuti unaoangalia mbele huhakikisha ushindani wa haki, kulinda wateja, na kuweka mazingira rafiki kwa sekta binafsi kushirikiana na waendeshaji wa huduma za posta. Tunapaswa kuoanisha sheria za posta na mifumo ya uchumi wa kidijitali. Ni muhimu kutafsiri upya dhana ya ‘Wajibu wa Huduma kwa Wote’ ili isihusishe tu usafirishaji wa barua, bali pia muunganisho wa kidijitali na upatikanaji wa huduma za kifedha,” alisema Dkt. Bakari.

Aliongeza kuwa kanuni bora zinaweza kuchochea ujasiriamali kwa kuruhusu wafanyabiashara wadogo kutumia miundombinu ya posta kwa ajili ya biashara mtandaoni na ya mipakani, na hivyo kuinua sekta zisizo rasmi na kuleta mifumo mipya ya mapato kwa waendeshaji wa huduma za posta.

Alisema ubunifu na usasa vinapaswa kwenda sambamba kwa kuwa mustakabali wa posta Afrika ni wa kidijitali unaotegemea takwimu kupitia mifumo ya kisasa.

“Ili huduma za posta ziendelee kuwa muhimu na zenye tija, ni lazima ziendane na teknolojia mpya kuanzia mfumo wa kumbukumbu kwa ajili ya miamala salama na ya uwazi, matumizi ya droni na magari ya umeme kwa usafirishaji wa haraka hadi matumizi ya programu za simu zinazowawezesha wateja kufuatilia vifurushi, kulipia huduma na kupata huduma muhimu kama vitambulisho vya kidijitali. Ubunifu huu si maboresho tu, bali ni njia za kuwawezesha wananchi kushiriki, kuongeza ufanisi na kujenga imani katika mifumo ya posta ya kisasa,” alisisitiza Dkt. Bakari mbele ya ukumbi uliojaa wadau kwenye Jengo la PAPU, Arusha.

Umoja wa Posta Afrika (PAPU) ulianzishwa tarehe 18 Januari 1980 jijini Arusha, Tanzania kama Taasisi maalum ya Umoja wa Afrika (AU) kwa lengo la kukuza huduma za posta barani Afrika. Ulipoanzishwa, PAPU ulikuwa na wanachama 35 pekee, lakini kwa sasa una jumla ya nchi wanachama 45. PAPU ilikuwa kiungo muhimu wakati wa harakati za ukombozi wa bara la Afrika na hivyo kuchangia pakubwa  katika ukombozi wa bara hili.

Mkutano wa 43 wa Baraza la Utawala la PAPU uliofanyika Arusha ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ndani nan je ya Afrka, akiwemo Mwenyekiti wa Baraza la Utawala la PAPU Bw. Abdelouahab Gbara, Katibu Mkuu wa PAPU Dkt. Sifundo Chief Moyo, Katibu Mkuu na Mwenyekiti wa Idara ya Posta, Serikali ya India Bi. Vandsta Kaul, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Umoja wa Posta Duniani (UPU) Bw. Marjan Oswald, na Naibu Katibu Mkuu wa PAPU Bi. Jessca Hope Sengooba.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!