JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Tanzania Ipo Tayari Kupokea Teknolojia ya Utangazaji Redio Kidijiti


Tanzania Ipo Tayari Kupokea Teknolojia ya  Utangazaji Redio...

Na Mwandishi Wetu

Mawimbi ya Utangazaji wa Redio nchini hivi karibuni yatajawa na sauti zenye ubora wa hali ya juu kufuatia hatua ya Serikali kukamilisha mkakati wa kuanzisha utangazaji wa kidijiti utakaoleta mapinduzi makubwa katika uwasilishaji wa huduma za utangazaji nchini.

Akizungumza kwenye mkutano wa mwaka wa utangazaji wa mwaka 2023 uliofanyika jijini Dodoma kuanzia tarehe 13 hadi 14 Februari 2024, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew alisema, Wizara ipo kwenye hatua za mwisho za kupitia Kanuni za Utangazaji zitakazoruhusu ujio wa teknolojia hiyo inayojulikana kama Digital Sound Broadcasting (DSB).

Naibu Waziri Kundo alieleza kuwa uamuzi wa kuikaribisha teknolojia ya utangazaji wa redio kidijiti unalenga kuleta utatuzi wa changamoto za sekta zikiwamo uhaba wa masafa ya utangazaji wa redio kwenye maeneo ya miji mikubwa ambayo hivi sasa inakabiliwa na uhaba wa rasilimali masafa.

Aidha ujio wa teknolojia hiyo utawezesha ufikishaji wa matangazo ya redio kwa hadhira pana zaidi kutokana na ukweli kwamba teknolojia ya utangazaji wa kidijiti haizuiwi na mipaka ya teknolojia, tofauti utangazaji wa redio wa sasa unaotegemea rasilimali masafa ili kufikisha maswasiliano kwa wananchi.

 

Akizungumzia ujio wa teknolojia hiyo Meneja wa Kitengo cha Huduma za Utangazaji TCRA Mhandisi Andrew Kisaka alieleza kuwa safa moja chini ya teknolojia hiyo litaweza kuzalisha vituo 14 vya utangazaji, hivyo kuwezesha ongezeko la idadi ya vituo vya utangazaji.

 

“Tunatarajia kwamba rasilimali moja ya masafa itawezesha vituo angalau 14 kutoa huduma, na hii itaondoa kikwazo cha ukosefu wa masafa hasa kwenye maeneo ya miji kama vile Dar es salaam, Mwanza, Dodoma na miji mingine,” alieleza.

Awali Naibu Waziri Kundo alisema Serikali imedhamiria kuhakikisha Utangazaji wa redio unawafikia watanzania wengi zaidi na kwamba Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari hivi sasa ipo kwenye hatua za mwisho kuidhinisha Kanuni za Utangazaji wa Redio zitakazotoa mwanya wa kuanza kutumika kwa DSB hapa nchini.

Mhandisi wa Teknolojia za Utangazaji nchini Sunday Mkayamba akizungumzia teknolojia hiyo alibainisha kuwa ni muhimu wadau wa sekta ya Utangazaji kuweka kipaumbele katika kuandaa maudhui yenye ubora wa hali ya juu kwa kuwa DSB italeta ushindani wa ubora wa maudhui.

Mkutano wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji huwaleta pamoja wadau wa sekta ya Utangazaji wakiwamo wamiliki wa vyombo vya Utangazaji, watangazaji, watozi, wakongwe wa sekta ya Utangazaji, taasisi za Serikali zinazohusiana na sekta ya Utangazaji na vituo vyote vya Utangazaji wa televisheni, redio, Utangazaji wa televisheni kwa njia ya waya, wakusanyaji na wasambazaji wa maudhui na zaidi. Mkutano wa mwaka 2023 ulibeba dhima ya Maadili katika sekta ya Utangazaji huku wakongwe wa sekta ya Utangazaji wakitoa wito kwa watoa huduma za Utangazaji kuzingatia kanuni za Utangazaji unaozingatia sheria, kanuni na miongozo.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!