TCRA, CAK NA KRA ZABADILISHANA UJUZI

Na Mwandishi wetu,
MAMLAKA ya mawasiliano Tanzania (TCRA) imekutana na kufanya kikao na maafisa toka Mamlaka za Mawasiliano (CAK) na Mapato (KRA) za kenya kwenye kikao kazi cha kubadilishana uzoefu juu ya usimamizi wa mifumo ya ndani ya mawasiliano inayowezesha kuchakata taarifa za Mapato za huduma za Mawasiliano. Kikao kazi hiko ni sehemu ya ziara ya siku tano ya Mamlaka hizo za kenya inayohusisha kutembelea ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA na TCRA.
Akiwakaribisha wageni hao toka Kenya kwenye ofisi za TCRA Mhandisi Andrew Kisaka aliyemuwakilisha Mkurugenzi Mkuu, alisema “Ni fahari kwetu kama mamlaka kuwapokea wataalamu wenzetu toka kwenye sekta hii, hii inaonesha namna ujirani wetu na nia njema ya Kukuza sekta ya mawasiliano kwenye kanda yetu…” mhandisi Kisaka aliwahakikishia kuwa ujio wao utanufaika sana na timu ya wataalamu toka TCRA waliojipanga kuwahudumia.
Ujumbe huo wa Maafisa 10, kutoka Kenya umeongozwa na Naibu Kamishna wa KRA ndugu Joseph Tonui alieambatana na Maafisa watano toka Mapato ya Kenya KRA, maafisa wanne toka Mamlaka ya Mawasiliano Kenya CAK na Afisa mmoja toka wizara ya Mawasiliano ya Kenya. Kamishna Tonui aliishukuru TCRA kwa kukubali ombi lao la kutembelea huku akieleza kuwa ziara yao inalengo la kujifunza na kuona namna Tanzania kupitia TCRA na TRA zinavyosimamia na kuchakata taarifa za mapato toka kwa watoa huduma za mawasiliano.
Akifanya wasilisho juu ya historia kuelekea kuanzishwa kwa mfumo wa usimamizi wa Mawasiliano Mhandisi Iddi Mtanga Meneja wa Kitengo cha TEHAMA; alieleza kuwa TCRA iliamua kusimamia na kutengeneza Mifumo yake yenyewe ya ndani na kuachana na utaratibu wa kutumia wazabuni kuunda na kusimamia mifumo hiyo. “Hapo awali tulikuwa na mfumo wa TTMS uliosimikwa na mzabuni ambao ulikuwa na uwezo wa kuchakata taarifa za makampuni ya simu pekee, lakini kwa sasa mfumo wa CMS ulioundwa na wataalamu wa ndani umeboreshwa na kuweza kuchakata mpaka huduma za Utangazaji na Posta…”
Nae Mhandisi Fuad Adam Meneja wa Kitengo cha Usimamizi wa Mifumo ya Mawasiliano CMS, alisema kwasasa mfumo wetu una modeli kumi na mbili ambazo zinachakata na kutoa taarifa kutoka kwa watoa huduma mbalimbali kuanzia watoa huduma za Simu, intaneti, Minara ya simu, utangazaji na wasambazaji wa vifurushi na vipeto ambapo inawezesha mamlaka kujua, kupanga na kuwashauri watoa huduma namna bora ya kuboresha huduma zao.
Kikao kazi hicho pia kilihusisha mjadala baina ya washiriki, akichangia mjadala huo Mhandisi Rodgers Mumelo toka Mamlaka ya Mawasiliano Kenya CAK alishauri namna TCRA inavyoweza ona namna ya kubadilishana uzoefu na wenzao wa Kenya kwa kutuma wataalamu elekezi kuona namna CAK inavyoweza kuachana na matumizi ya program zinazoundwa na kuratibiwa na wazabuni na kuwa na uwezo kupitia wataalamu wa ndani.
Akijibu hoja hiyo Mhandisi Iddi Mtanga alisema TCRA imefanya jitihada za makusudi kuajiri na kuendeleza wataalamu wake yenyewe ili kulinda taarifa zake na za nchi, kupunguza gharama za kulipa wazabuni, kuwa na mifumo endelevu isiyotegemea watu wa nje ambao mara nyingi hawawezi kukidhi vigezo vya mikataba. Pia aliongeza kuwa TCRA imekuwa na itaendelea kupokea wageni toka mataifa mbalimbali wanaopenda kujifunza namna inavyosimamia mifumo yake.
Akitoa neno la shukrani Naibu Mkurugenzi Tanui alisema “Nawapongeza sana TCRA kwa hatua kubwa sana mliyofikia katika kuhakikisha mmejenga uwezo wa ndani wa taasisi lakini kwa kuwa na mifumo bora na salama iliyopunguza gharama na hatari ya udukuzi..
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imeendeleza utamaduni wake wa kupokea na kutoa elimu kwa mataifa jirani yanayokuja kwa lengo la kujifunza na kuboresha mifumo yao ya Huduma. Hii ni sera nzuri katika kujenga mahusiano mazuri na kukuza maendeleo ya TEHAMA nchini, pia ianendana na sera za serikali ya awamu ya sita katika kufungua mipaka na kukuza uchumi hasa katika zama hizi za uchumi wa kidijiti.