JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Kamati ya Maudhui ya TCRA Yatahadharisha Maudhui yasiyofaa katika Vyombo vya Utangazaji


Kamati ya Maudhui ya TCRA Yatahadharisha Maudhui yasiyofaa k...

 

Na Mwandishi Wetu

Kamati ya maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa tahadhari kwa vyombo vya Utangazaji nchini kuzingatia urushaji wa maudhui yenye kuzingatia maadili ili kuilinda jamii dhidi ya maudhui yasiyofaa.

Taarifa ya Kamati iliyotolewa Agosti 29, 2022 ilieleza kuwa, siku za hivi karibuni kumekuwa na taarifa inayosambazwa na baadhi ya watumiaji wa mitandao ya Kijamii ikitahadharisha juu ya uwepo wa maudhui ya televisheni kwenye vipindi vya watoto yaliyo kinyume na Sheria, Kanuni za Utangazaji, Maadili na Miiko ya utangazaji nchini.

Katika ufafanuzi wake Kamati ilieleza kuwa uchunguzi umebaini kutokuwepo kwa taarifa zisizofaa kupitia vipindi tajwa na kuongeza “TCRA inapenda kuuhakikishia umma kuwa vipindi vya maudhui vyote vinayorushwa na vyombo vya Utangazaji hapa nchini huhakikiwa kwanza na pia kufuatiliwa ili kujiridhisha kuwa yanazingatia Sheria, Kanuni, Maadili na Utamaduni wa Mtanzania,” ilifafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa Mamlaka ya Mawasiliano imejiridhisha kuwa, hakuna chombo cha Utangazaji kilichorusha maudhui yasiyofaa kwa watoto. Hata hivyo, TCRA inavikumbusha vyombo vyote vya Utangazaji kuendelea kuzingatia matakwa ya Sheria, Kanuni na Masharti ya Leseni ya Utangazaji kwa kuhakikisha vituo vyao haviendi kinyume na maadili ya kitanzania.

“Aidha, TCRA inaendelea kusisitiza kuwa wajibu wa kuwalinda Watoto kutokana na maudhui yasiyofaa hasa kwenye mitandao ya kijamii ni wa kwetu sote ikianzia kwa Wazazi, Walezi na Mashuleni ambapo Watoto wetu hutumia muda mwingi huko wakiwa masomoni,” iliongeza taarifa hiyo.

Pia TCRA inaiasa jamii kutosambaza katika mitandao ya kijamii jumbe zinazoleta taharuki, upotoshaji na hofu katika jamii. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wale wote watakaobainika kusambaza jumbe hizo. TCRA inafuatilia kwa ukaribu maudhui yanayowekwa kwenye mitandao. Kwa yeyote atakayebainika kuweka na kusambaza habari za upotoshaji mitandaoni, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imepewa jukumu la kusimamia maudhui yote yanayorushwa na vituo vya Utangazaji pamoja na mitandao ya ki-elektroniki.

MWISHO

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!