JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Tanzania Kisima cha Mafunzo ya Mawasiliano


Tanzania Kisima cha Mafunzo ya Mawasiliano

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeendelea kuwa kisima cha mafunzo ya mawasiliano kwa nchi nyingine za Afrika.

Ujumbe wa wataalamu wa mawasiliano kutoka Tume ya Mawasiliano ya Eswatini (ESCCOM) hivi majuzi ulifika katika ofisi za makao makuu ya TCRA kushiriki katika mafunzo ya siku mbili ya Sekta ya Utangazaji.

Wataalamu hao kutoka Eswatini walifika TCRA kujifunza kuhusu Mifumo ya Utangazaji, Utoaji leseni za utangazaji, na mwelekeo wa Sekta ya Utangazaji wa Televisheni na Redio kuanzia tarehe 9 hadi 13 Oktoba 2023.

Ujumbe huo ulioongozwa na Vusi Khumalo, Meneja wa Utangazaji Tume ya Mawasiliano ESCCOM, ulitoa shukrani kwa TCRA kwa ushirikiano na uzoefu waliopata, ambao wamesema utaenda kuimarisha utendaji wao.

“Tumeona jinsi TCRA ilivyowekeza katika mifumo ya kutazama na kufuatilia matangazo pamoja na utoaji wa leseni kwa mtandao,” alisema Khumalo.

Walipowasili katika makao makuu ya TCRA jijini Dar es Salaam, ujumbe huo kutoka Eswatini ulikaribishwa na Ndugu John Daffa, Mkurugenzi wa Leseni na Ufuatiliaji, ambaye aliwakaribisha kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt Jabiri Bakari.

Baada ya kupokelewa na utambulisho, wataalamu wa vitengo mbalimbali vya TCRA walishirikiana na wageni hao kwa kubadilishana uzoefu na ujuzi wa uendeshaji wa sekta.

Tanzania, kupitia Mamlaka ya Mawasiliano, imekuwa nchi muhimu kwa kutoa mafunzo kwa wageni kutoka mataifa mbalimbali wanaojifunza masuala mbalimbali ya sekta ya mawasiliano zikiwemo Mamlaka za usimamizi wa sekta ya mawasiliano Kusini, Magharibi na Kaskazini mwa bara la Afrika.

Wataalamu kutoka Eswatini ni wageni wa pili kupokelewa na TCRA mwezi wa Oktoba 2023, wakifwatia wageni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano na Huduma za Posta Mali (AMRTP) mwezi huo huo.

Mwezi Septemba 2023, TCRA ilipokea ujumbe mwingine kutoka Mamlaka ya Mawasiliano nchini Msumbiji (INCM) uliofika Tanzania kujifunza masuala mbalimbali, ikiwemo utoaji wa leseni.

Nchi nyingine ambazo zimenufaika na mafunzo ya kubadilishana uzoefu kwa kuleta wataalamu nchini Tanzania kupitia TCRA ni Malawi, Msumbiji, Zambia, Botswana, Rwanda, Mali na Burundi.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!