JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

TCRA yashirikisha wadau kuleta Ufanisi, Huduma za Utangazaji na Posta


TCRA yashirikisha wadau kuleta Ufanisi, Huduma za Utangazaji...

Na Mwandishi wetu

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inashirikiana na wadau mbalimbali Kuboresha maudhui ya utangazaji nchini ili kulinda tunu za taifa, na pia kupanua wigo wa utoaji wa huduma za posta.

Taarifa ya TCRA ya Oktoba hadi Disemba 2023, iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt. Jabiri K. Bakari imetaja hatua hizo za uboreshaji kuwa ni pamoja na kuhimiza uandaaji wa maudhui yanayozingatoia maadili ya Kitanzaniia, na kanuni. Vilevile mafunzo yametolewa kwa  watoa huduma za posta.

Dkt. Bakari amefafanua kwamba utangazaji ni njia pekee ya Mawasiliano inayowafikia watu wengi kwa haraka na wakati mmoja na kuongeza kwamba TCRA ina wajibu wa kuweka mazingira rafiki ya kusambaza huduma za Utangazaji kwa njia ya redio, televisheni na mitandao nchi nzima ili kumfikia kila mwananchi.

Taarifa imeainisha hatua zinazochukuliwa na TCRA kuhakikisha kuwa Maudhui yanayorushwa na vituo vya Utangazaji yanazingatia maadili na weledi wa uandishi wa habari na pia hayakiuki Sheria na Kanuni.

Dkt. Bakari ameeleza kwamba TCRA inahimiza utengenezaji, uzalishaji na usambazaji wa maudhui ya ndani) na kutangaza urithi, vivutio, mila na desturi za Mtanzania.

TCRA imeandaa vipindi maalumu vya redio vitakavyotoa elimu kuhusu uzingatiaji wa maadili, mila, desturi na Utamaduni wa Mtanzania. Vipindi hivyo vilizinduliwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa Desemba 2023. Kwa kuanzia vitarushwa na vituo 150 vyenye leseni ya kiwilaya ya utangazaji wa redio.

Dkt. Bakari ameongeza kwamba TCRA inashirikiana na waandaji binafsi wa maudhui ya ndani ili kuandaa maudhui ya yenye ubora.  Mipango imekamilika kuwezesha utoaji mikopo kwa masharti nafuu kwa watengenezaji maudhui binafsi na vituo vya Utangazaji ili kukabiliana na changamoto ya raslimali fedha kwa watu wenye vipaji vya kuandaa maudhui bora ya ndani, ameeleza.

Taarifa pia imedokeza kwamba TCRA kwa kushirikiana na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Chuo Kikuu cha Dodoma imeendelea kuratibu kazi ya kurekodi ngoma za asili za makabila 120 kwa ubora wa hali ya juu ili kukuza utamaduni wa Tanzania.

Mpaka sasa makabila 10 ya Kitanzania yamerekodiwa. Wataalamu wa masuala ya historia za makabila wataandika makala yanayohusu kila kabila ili kuwa na kumbukumbu ya vizazi vyote. Zoezi hili litafanyika kwa awamu nne”, amebainisha Dkt. Bakari.

Ikitoa picha ya matumizi ya huduma za utangazaji wa kidijital, taarifa imeonesha ongezeko la matumizi ya visimbuzi au dekoda za utangazaji wa televisheni wa kidijitali kwa mifumo ya ardhini satelaiti na waya. 

Visimbuzi 3,661,976 vilikuwa hewani hadi Disemba 2023 ikilinganishwa na visimbuzi 3,631,649 mwezi Septemba 2023. Kati ya hivyo, 1,781,340 ni vya dijitali kwa mfumo wa televisheni wa utangazaji wa mitambo ya ardhini na 1,880,636 ni vya mfumo wa televisheni wa satelaiti.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Dar es Salaam inaongoza kwa kuwa na visimbuzi (1,400,260), ikifuatiwa na Arusha (291,605), Mwanza (289,598) na Mbeya (227,737). Mkoa wenye visimbuzi vichache ni Songwe (1,570).

Huduma ya televisheni kwa waya zimeenea mikoa ya Kanda ya Ziwa; ambapo Shinyanga unaongoza; ukiwa na jumla ya waliounganishwa 2,803, ikifuatiwa na Mwanza, yenye 2,195 na ya tatu ni Kagera ikiwa na waliounganishiwa 1,770.

Mikoa yenye wateja wachache ni Kilimanjaro (130), Morogoro (120) na Pwani iliyounganisha wateja 30.

TCRA, ambayo inasimamia pia sekta ya posta, imetoa leseni 116 zikiwa ni kwa Shirika la Posta Tanzania na watoa huduma wengine wa kusafirisha vifurushi na nyaraka.

Leseni zilizotolewa hadi Desemba kwa makundi matano ya watoa huduma imeongezeka. leseni hizo ni sita za watoa huduma kimataifa, moja kwa mtoa huduma afrika mashariki, 45 kwa watoa huduma ndani ya mipaka ya Tanzania, 14 kwa watoa huduma ndani ya mji mmoja na 50  kwa watoa huduma wanaotumia mabasi ya abiria.

Mamlaka pia inatekeleza mipango kadhaa ya kubadili mwelekeo wa huduma za posta. Hatua zilizochukuliwa katika maboresho ni pamoja na kutoa mafunzo kwa watoa huduma za usafirishaji wa vifurushi na vipeto kuhusu umuhimu wa matumizi ya anwani za makazi na postikodi, usalama na umakini.

Mafunzo hayo yaliyotolewa kikanda, yalilenga  kuzuia kusafirisha vitu hatarishi  katika mnyororo wa usafirishaji wa vifurushi na vipeto..

Huduma za Shirika la Posta pia zinaboreshwa kwa kushirikiana na Umoja wa Posta Duniani (UPU) kwa kuimarisha mfumo wa kusimamia Ubora wa Huduma za Posta katika ofisi za Posta Zanzibar, Mikoa ya Dar es salaam, Arusha, Kigoma, Mwanza, Dodoma na Mbeya.

Mfumo huu utawezesha ufanisi katika usimamizi na udhibiti wa ubora wa huduma, Dkt. Bakari amefafanua.

TCRA ilishirikisha wadau wa Sekta ya Posta Kanda ya Mashariki ambapo mwelekeo wa Umoja wa Posta Duniani ulijadiliwa. Mwelekeo huo ni kuifungua UPU kwa wadau wengine zaidi wanaotoa huduma mbalimbali zinazoambatana na zile zinazotolewa na Sekta ya Posta  moja kwa moja. Tanzania itakuwa mwenyeji wa Kituo kikubwa cha TEHAMA (ICT) kitakacho gharamiwa na Umoja wa Posta Duniani (UPU) kwenye Jengo la PAPU jijini Arisha, kikihudumia Nchi wana chama wa PAPU wapatao 45.

Dkt. Bakari ameeleza kuwa kufunguliwa kwa UPU kunafuatia mageuzi ya sekta ya posta, ambayo yamesababishwa na kuwepo kiwango kikubwa cha mwingiliano wa huduma za posta na huduma nyingine, ubinafsishaji wa mashirika ya posta na kuongezeka kwa shughuli za biashara ya mtandao duniani.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!