JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

TCRA yazindua Kampeni kutokomeza Utapeli Mtandaoni


TCRA yazindua Kampeni kutokomeza Utapeli Mtandaoni

 

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imezindua kampeni ya elimu kwa umma ikiwa na lengo la kuwakumbusha na kuwaelimisha watumiaji wa huduma za mawasiliano na wananchi umuhimu wa kutumia huduma hiyo kwa umakini ili kuepuka wizi na ulaghai wa kimtandao.

Kampeni hiyo imezinduliwa siku chache baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dk Jabiri Bakari kusisitiza dhamira ya taasisi anayoisimamia na kuiongoza inahakikisha mazingira ya kimtandao yanakuwa salama, ili yawe yenye kuchangia ukuaji wa uchumi wa kisasa yaani Uchumi wa Kidijitali.

“TCRA tumedhamiria kuhakikisha mtandao unakuwa sehemu salama zaidi na unaleta matokeo chanya katika uchumi wa taifa letu,” alisisitiza Dk Bakari na kuongeza.

"Mtandaoni ni mahali ambapo tuna fursa nyingi; matumizi mazuri ya majukwaa haya ya kimtandao yanaweza kutambua fursa chanya za kufungua faida nyingi zinazopatikana kwenye mazingira haya ya kisasa ya kimtandao" alibainisha.

Akizungumzia kampeni hiyo Mkuu wa Kitengo cha TCRA, Lucy Mbogoro alisisitiza kuwa TCRA imejidhatiti kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na elimu ya matumizi sahihi na salama ya mitandao yenye kuleta tija.

"Mamlaka ya Mawasiliano tumeona ni vema wananchi waendelee kuwa na uelewa mpana wa kuepuka utapeli wa mtandao ndio sababu tumekuja na kampeni", alisema Mbogoro

Mbogoro alisema kuwa kampeni hiyo imejikita kuwaelekeza watumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu kuhakiki laini zao za simu kwa kubofya *106# kisha kufuata maelekezo kwani kwa kufanya hivyo wataweza kuhakiki namba za simu za mitandao yote zilizosajiliwa kwa namba ya kitambulisho chake cha Taifa (NIN). Aliongeza kuwa ikiwa mtumiaji huduma za Mawasiliano atabaini uwepo wa namba za simu asizozitambua basi atalazimika kufika kwa Mtoa Huduma wa mtandao anaotumia ili azifute namba hizo asizozitambua.

"Zoezi hili la uhakiki ni muhimu sana kwa kuwa linamwezesha mtumiaji huduma za mawasiliano kuwa salama; huwezi kujua ni nani anaetumia laini zako, vipi je, akitenda jinai!? Utasalimika, hivyo nawasihi watanzania wenzangu wahakiki laini zao za mawasiliano, ni muhimu sana"

Mbogoro aligusia kuhusu utapeli unaotumwa kwa njia ya ujumbe mfupi ukimtaka mtumiaji huduma kutuma fedha na aina nyingine za jumbe zenye viashiria vya kitapeli alisisitiza kuwa, mtumiaji anapaswa kuandika neno Utapeli kisha kulituma kwenda namba 15040 na kufuata maelekezo ikiwa ni pamoja na kuweka namba za simu za mshukiwa wa utapeli, akisisitiza kuwa kwa kufanya hivyo mtumiaji huduma atakuwa mojakwamoja ametoa taarifa ya utapeli kwa kikosikazi kinachoshughulikia utapeli mtandaoni. "Ukitoa taarifa kwenye namba hiyo mojakwamoja kikosi-kazi hiki kinafuatilia na utapokea mrejesho" alibainisha Mbogoro.

Meneja wa Watumiaji na Wateja wa TCRA, Thadayo Ringo alisisitiza kuwa kampeni hiyo ni muhimu kupunguza mashauri ya watumiaji huduma za mawasiliano kutapeliwa.

"Tumekuwa tukisisitiza kwamba mtumiaji huduma mara zote asitoe kabisa ushirikiano kwa mtu yeyote asiemfahamu mara anapofikiwa kwa njia ya simu, iwe kwa ujumbe mfupi, sauti au mitandao ya kijamii. Kwa mfano ukitumiwa link usiyoifahamu, usifungue; mtu akikupigia kukuarifu kuhusu ushindi wa bahati nasibu ambayo hujashiriki,au wale wanaosema mwanao ni mgonjwa shuleni na wengine kama hao, usiwape ushirikiano, kuepuka kutapeliwa," alisema Ringo.

Ringo alisema watumiaji huduma wanaonuia kununua bidhaa mtandaoni kuhakikisha wanajiridhisha na uhalali wa muuzaji ikiwemo kufahamu anwani zao halisi na usajili wao kabla ya mtu kufanya maamuzi ya kufanya manunuzi kwa njia ya mtandao.

“Hivi karibuni tumesikia baadhi ya watumiaji majukwaa ya biashara mtandao wakitapeliwa, nawaomba watumiaji huduma za maduka-mtandao kuongeza umakini hasa wale wanaoagiza mizigo ya biashara nje ya nchi bila wao kwenda wanaweza kutumia ofisi zetu za Tanzania zilizopo huko ng'ambo ili kujiridhisha na uhalali wa maduka-mtandao hayo, ili kuepuka kupoteza rasilimali fedha kwa kutuma fedha kwa matapeli wa mtandaoni," alieleza Ringo.

Ringo alisema wanunuaji bidhaa mitandaoni ni vema wakafuatilia kujua ikiwa duka-mtandao la nje ya nchi lina wakala wake hapa nchini, na anunue kupitia wakala, badala ya kuagiza mojakwamoja hasa ikiwa anapaswa kufanya manunuzi makubwa kama vile biashara.

Kampeni hiyo ya TCRA inaongozwa na jumbe mbalimbali za elimu kwa umma zinazosisitiza; usitume pesa kwa mtu usiyemfahamu; hakiki ujumbe na namba inayokutaka utume pesa kabla ya kufanya muamala;mawasiliano baina ya mteja wa huduma za mawasiliano ya simu na mtoa huduma wake ni kuptia namba 100 pekee; epuka maelekezo yanayotolewa kupitia namba binafsi kuhusiana na huduma za mawasiliano ya simu; epuka kufungua link za mtandaoni usizozifahamu; usichapishe chochote kuhusu watu wengine bila ridhaa yao; zuia (block) mtu yeyote anayetuma maoni ya kukusumbua, kukutishia au yasiyofaa kuhusu wewe; toa taarifa kwa Jeshi la Polisi iwapo utapata shambulio la mtandaoni; na matumizi salama ya mtandao yanachangia katika maendeleo ya uchumi, miongoni mwa jumbe.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!