JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

TCRA Yazindua Kitabu cha Kuanzisha na Kuratibu Klabu za Kidijiti ili Kukuza Ubunifu kwa Vijana


TCRA Yazindua Kitabu cha Kuanzisha na Kuratibu Klabu za Kidi...

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Alhamisi, Novemba 2, 2023, ilizindua kitabu cha Kuanzisha na Kuratibu Klabu za Kidijiti ili kurahisisha kuanzishwa na uratibu wa klabu za kidijiti katika shule, vyuo na vyuo vikuu nchini.

Hafla ya uzinduzi, ambayo ilifanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Maktaba Kuu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, iliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari na Mawasiliano, Mhe. Mohammed Khamis Abdulla.

Katika hotuba yake, Mhe. Abdulla alisema kuwa Serikali iko katika mchakato wa kukamilisha Sera ya Ubunifu itakayohakikisha wabunifu wa teknolojia za kidijiti wananufaika na kuwa washiriki wenye tija katika kuijenga Tanzania ya Kidijitali.

Katibu Mkuu alisisitiza kuwa klabu za kidijiti zina jukumu muhimu katika kuhimiza wanafunzi kujifunza na kuyapenda masomo ya STEM (sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati) ambayo yana umuhimu mkubwa katika kukuza ujuzi wa uchumi wa kidijitali unaohitajika  ili kufanikiwa kujenga Tanzania ya kidijitali.

Aliipongeza TCRA kwa kuandaa Kitabu hicho cha Kuanzisha na Kuratibu Klabu za Kidijiti, ambacho kitatoa mwelekeo kwa shule, vyuo na vyuo vikuu juu ya namna ya kuanzisha na kuendesha klabu za kidijiti.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Jabiri Bakari alisema kuwa kitabu hicho kitawawezesha wanafunzi na vijana kujifunza na kukuza ujuzi katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na hatimae kuwa washiriki halisi wa ujenzi wa uchumi wa kidijitali.

Alisema kuwa klabu za kidijiti zitawasaidia wanafunzi kuwa raia wa kidijitali wenye uwajibikaji na kuchangia maendeleo ya Tanzania ya kidijitali.

Dkt. Bakari alisema kuwa TCRA ilianzisha wazo la Klabu za Dijiti katika Vyuo na Vyuo Vikuu mwaka 2022, na kwamba mpango huo tangu wakati huo umepanuliwa kujumuisha vyuo na vyuo vikuu na sasa unatarajiwa kupanuliwa hadi taasisi zote za elimu.

Alisema kuwa TCRA inashirikiana na TAMISEMI, Wizara ya Elimu, TCU na NACTVET ili kuhakikisha kuwa taasisi za elimu kote Tanzania zinaunga mkono mpango wa klabu za kidijiti kwa shabaha ya kuchagiza maendeleo ya uchumi wa kidijitali na buluu Tanzania.

Kitabu hicho kinajibu maswali yafuatayo:-

  • Klabu ya kidijiti ni nini?
  • Kwa nini uanzishe klabu ya kidijiti?
  • Jinsi ya kuanzisha klabu ya kidijiti
  • Jinsi ya kuendesha klabu ya kidijiti
  • Shughuli za klabu ya kidijiti
  • Rasilimali za klabu za kidijiti

Wakati wa hafla ya uzinduzi, Katibu Mkuu pia alizindua tovuti ya usajili wa klabu za kidijiti ambayo wanafunzi wanaweza kusajiliwa, tovuti hiyo inapatikana kupitia https://digitalclubs.tz/.

Bakari aliorodhesha faida za Klabu za kidijiti kwa wanafunzi kuwa ni pamoja na:

  • Kuongeza uelewa wa TEHAMA na uchumi wa kidijitali
  • Fursa ya kukuza ujuzi wa TEHAMA
  • Klabu ni fursa ya kujifunza kuhusu  ushiriki kwenye uchumi wa kidijitali
  • Fursa za kuchangia maendeleo ya Tanzania ya kidijitali

Klabu za dijitali pia zinawapa wanafunzi jukwaa la kuwasiliana na wanafunzi wengine wanaopenda TEHAMA na Teknolojia za kidijiti, kushirikiana katika miradi na kujifunza kutoka kwa wengine wakiwemo wataalamu wa sekta ya teknolojia za kidijiti.

Goodluck Paul mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kuwa uzinduzi wa kitabu hicho ni hatua chanya kuelekea kukuza ubunifu wa vijana na maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!