JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

TCRA yaelimisha wadau mipango kusimamia Taka za Ki-elektroniki


Na mwandishi wetu

HATUA zilizochukuliwa na Tanzania kuanzia mwaka jana kuhusu utupaji salama wa taka za kielekroniki zinalenga kulinda afya za watu na mazingira, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Dkt. Jabiri Bakari amebainisha.

Ameeleza kwamba ukaguzi wa awali na ukusanyaji wa ada ya mazingira kuanzia Mei 2023 kwa vifaa vya mawasiliano vinavyoingizwa Tanzania unalenga kusimamia utupaji wa vifaa hivyo mwisho wa matumizi yake bila kudhuru afya za watu na mazingira.

Dkt. Bakari alikuwa akiongea na wawakilishi wa Chama cha Wafanyabiashara wa Kariakoo ambao walialikwa TCRA hivi karibuni kwa kikao cha mashauriano, kama sehemu ya Mamlaka ya kusimamia sekta kwa kushirikisha wadau.

Kariakoo ni kitovu cha biashara za vifaa vya waagizaji na watumiaji huduma za mawasiliano ya Ki-elektroniki,Tanzania.

Bakari aliwafahamisha wafanya biashara hao kuhusu hatua TCRA ilizochukua kusimamia taka elektroniki chini ya Kanuni za mwaka 2020 kuhusu Viwango vya Vifaa na  Usimamizi wa Taka Elektroniki.

Tanzania inasimamia utupaji wa taka elektroniki. Inahimiza utupaji sahihi na salama ili kuzuia vijenzi hatarishi na vyenye sumu vilivyomo kwenye vifaa vya mawasiliano visiathiri afya ya binadamu na mazingira.

Ada ya mazingira ilianzishwa kuwezesha usimamizi wa utupaji taka zitokanazo na vifaa vya mawasiliano vya kielektroniki.

Eco Levy, inawapa watengenezaji uwajibikaji wa kuhakikisha vifaa vyao vinatupwa kwa usahihi. Vifaa vyote vya mawasiliano vinavyoingia Tanzania vinakaguliwa kwenye nchi vinakotoka.

 Vilevile, vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki vinavyoingia Tanzania vinatakiwa kuidhinishwa na TCRA. Mamlaka pia inatoa leseni za uagizaji na usambazaji wa vifaa vya mawasiliano.

Kanuni za mwaka 2021 za Usimamizi wa vifaa vya umeme na elektoniki zinawataka waagizaji wa vifaa hivyo kulipa ada ya mazingira kabla havijasafirishwa kuja Tanzania.

Kanuni hizo zinahusu hatua zote za vifaa vilivyoagizwa. Hizi ni pamoja na uagizaji, usambazaji, uuzaji, uchakataji, ukarabati, uundaji, ufumuaji na utupoaji wa taka za vifaa vya umeme na vya kielektroniki Tanzania.

Tanzania inafuata kanuni na misingi ya kimataifa katika usimamizi wa taka elektroniki.

Usajili na ukaguzi wa vifaa vya mawasiliano  kwenye nchi vinakotoka unazingatia  masharti ya Mkataba wa Basel kuhusu usafirishaji wa taka hatarishi nje ya mipaka ya nchi na utupaji wa taka hizo, baada ya matumizi yake kufikia kikomo.

Mkutano wa TCRA na wawakilishi wa wafanyabiashara Kariakoo ni sehemu ya kampeni ya Mamlaka ya kuongeza uelewa wa wadau kuhusu utupaji salama wa taka elektroniki. TCRA inaongoza sekta ya Mawasiliano kwa kushirikisha wadau katika masuala muhimu ya maendeleo ya sekta.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!