TCRA YATOA WITO KWA VYUO VIKUU KUBORESHA MITAALA YA TEHAMA

Na Mwandishi wetu
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt Jabiri Bakari ametoa wito kwa vyuo vya elimu ya juu nchini kuangalia mitaala yao ya elimu ya TEHAMA na Uhandisi ili kuweza kuzalisha wataalamu wenye ujuzi na weledi wa hali ya juu. Hayo ameyasema jana jijini Dodoma wakati akifunga shindano la Masuala ya Usalama Mtandaoni kutoka vyuo mbalimbali nchini.
Shindano la kuwatafuta vinara wa Kubuni Mifumo ya kukabiliana na changamoto za Usalama Mtandaoni linaratibiwa na TCRA kwa lengo la kuibua na kukuza uwezo kwa vijana, kuimarisha na kukabili vihatarishi vya usalama mtandaoni na kushiriki kikamilifu kwenye uchumi wa kidijiti. Shindano hili linafahamika kama “Cyber Champions 2025” lilishirikisha washiriki 697 kutoka vyuo 43 nchini.
Dkt. Jabiri alipongeza washiriki wote waliofanikiwa kujisajili na kushiriki kwenye shindano la mwaka huu. “Kwa vijana wa umri wenu kuweza kutambua umuhimu wa TEHAMA na kuwekeza muda wenu kujisajili na kushiriki hata kama hamjashinda ila ni hatua ya kujitambua na kushiriki kwenye kujenga uchumi endelevu wa kidijiti” aliwaeleza washiriki.
Mbali na pongezi hizo, Dkt. Jabiri alioneshwa kutoridhishwa na idadi ndogo ya vyuo na washiriki walioweza kufika hatua za juu za mashindano la waka huu. Kutoka idadi ya washiriki 697 kutoka vyuo 43 walianza shindano, washiriki 247 kutoka vyuo 16 walifanikiwa kungia hatua ya nusu fainali, ambapo washiriki 50 kutoka vyuo vinne (4) ndio walifanikiwa kuingia fainali; “hii sio ishara nzuri kwa maandalizi ya vijana hawa wanaoshiriki kwa idadi ya vyuo 43, ni vyuo vinne tu ndo vimeweza kufika hatua ya fainali,hapa kuna shida mahali vyuo vyetu vina homework ya kufanya…”
Aliongeza kuwa Taasisi za elimu zina kitu cha kubeba kutokana na takwimu za mashindano haya maana hizi namba zinaongea vitu vingi ambavyo vyuo vyetu vinapaswa kuvifanyia kazi. Maandalizi ya vijana wetu hasa katika zama hizi za uchumi wa kidijiti yanapaswa kuzingatia mahitaji ya wakati husika na kujiendeleza mara kwa mara kwakuwa teknolijia inabadilika kila siku.
“ Katika kuwakuza vijana wetu kwenye mfumo wa elimu huko vyuoni inabidi tuwaandae vijana ambao wataweza kuingia kwenye soko la ushindani kupata ujuzi utakaowawezesha kuwa wabunifu na kutoa majawabu na suluhu ya masuala mbalimbali yanayohusisha maisha ya kila siku,” Alieleza. Dkt. Jabiri alisema, Uchumi wa kidijiti ni aina ya uchumi unaohitaji akili iliyoandaliwa katika muda sahihi na hili linahitaji vijana walioandaliwa vizuri katika vyuo vyetu na hata kwenye elimu za chini.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, alikazia pia umuhimu wa kushiriki katika klabu za kidijiti hasa kwa kuzingatia vilabu hivi vinawajenga vijana wabunifu, mahiri na wabobevu katika maeneo ya TEHAMA. Msingi mkubwa wa kuwa vijana mahiri kwenye TEHAMA huanzia shuleni kwa kusoma masoma ya STEM (Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati) kwahiyo tunawasisitiza wenzetu kwenye sekta ya elimu kuwajenga vijana kwenye eneo hili la STEM.
Kauli ya Dkt. Jabiri inakuja wakati ambapo Tanzania inajitahidi kuimarisha uchumi wake wa kidijitali kwa kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu katika sekta ya TEHAMA. Wito wake unatoa msukumo kwa vyuo vikuu kuchukua hatua madhubuti katika kuandaa kizazi kijacho cha wataalamu wabobezi wa teknolojia