JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

TCRA Yashuhudia Utiaji Saini Mkataba wa Kuimarisha Huduma za Mkongo nchini Burundi


TCRA Yashuhudia Utiaji Saini Mkataba wa Kuimarisha Huduma za...

Na Mwandishi Wetu

Dar es Salaam, Tanzania, Februari 23, 2024 - Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt. Jabiri Bakari, ameshiriki katika tukio la utiaji saini wa makubaliano ya biashara kati ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Taasisi ya Burundi Backbone System (BBS). Mradi huu unalenga kuongeza ufanisi wa huduma kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wa Burundi kupitia Mkataba wa Biashara wa miaka mitano wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 3.3/- sawa na Shilingi za Kitanzania Bilioni 8.3/.

Utiaji saini huo ulifanyika jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa hoteli ya Johari Rotana na kuongozwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Moses Nnauye. Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga, alieleza kuwa Burundi, kupitia Taasisi ya Burundi Backbone System (BBS), imeamua kuongeza mahitaji ya huduma za mkongo wa mawasiliano kutoka Tanzania kutokana na mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa mashirikiano ya kiteknolojia baina ya Tanzania na Burundi mwaka 2019.

“Tunajivunia uhusiano wetu tangu mwaka 2019… Baada ya matokeo mazuri ya huduma za Mkongo wa Taifa, jirani zetu Serikali ya Burundi kupitia Burundi Backbone System imekubali kuongeza huduma kutoka kwenye Mkongo wa Taifa wa mawasiliano, kwa Mkataba wa Kibiashara wa Miaka Mitano,” alisema Ulanga.

Kwa kutambua mchango wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mtendaji Mkuu wa BBS, Bw. Jeremie Diomede Hageringwe, baada ya utiaji saini wa Mkataba wa Huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, alimkabidhi zawadi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Dkt. Jabiri Bakari.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaendelea kuwa mshirika muhimu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mawasiliano nchini Burundi. Mwezi Novemba 2021, Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Posta wa Burundi, Bi. Lea Ngabire, pamoja na wataalamu wa mawasiliano, walitembelea Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kwa ziara ya mafunzo. Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri Bakari, aliahidi kuendeleza ushirikiano wa kitaalamu baina ya Mamlaka hizi mbili za usimamizi wa mawasiliano.

Tanzania ni mshirika muhimu katika usambazaji wa huduma za mkongo wa mawasiliano kwa nchi za Afrika Mashariki, na Burundi ni miongoni mwa nchi zinazonufaika na ushirikiano huo wa kiteknolojia kwa kuunganishwa na Mkongo wa Mawasiliano kutoka Tanzania. Nchi nyingine miongoni mwa nyingine zinazonufaika ni pamoja na Rwanda, Congo DRC, Malawi, na Msumbiji.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!