TCRA yasukuma Mageuzi Sekta ya Posta
Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inapitia upya mfumo wa kisheria na usimamizi wa sekta ya Posta ili kuwezesha uanzishwaji wa aina mpya za biashara, imefahamika.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt Jabiri Bakari amesema hatua hiyo inaenda sambamba na kuhakikisha uzingatiaji wa viwango vya ubora wa huduma na kuhakikisha uendelevu wa sekta kwa muda mrefu.
Ameeleza kuwa TCRA inatambua kwamba ukuaji endelevu wa shughuli za posta na usafirishaji vifurushi unatakiwa kuimarishwa na kanuni imara zinazozingatia masuala ya jamii, mazingira na utawala.
“Kujumuisha masuala haya katika mfumo wa usimamizi ni muhimu ili kuhakikisha kuwa sekta inaendelea kuwa stahimilivu, jumuishi na inayokabiliana na changamoto zinazojitokeza kwenye teknolojia, uchumi na mazingira”, Dkt Bakari ameeleza.
Dr Bakari ameielezea sekta ya posta kama mwezeshaji muhimu wa uchumi wa kidijitali Afrika kupitia matumizi ya TEHAMA kutokana na nafasi yake kwenye kufanikisha biashara mtandao.
“Kadri biashara ya mtandaoni inavyoendelea kupanuka, Sekta ya Posta ina majukumu muhimu katika kuunganisha biashara na watumiaji, kuwezesha biashara mipakani, na kuhakikisha kuwa vitu vya posta vinafikishwa kwa uhakika kwa wenyewe, hasa walioko vijijini na jamii kwenye maeneo yasiyofikiwa na huduma kikamilifu.”
Aidha ameongeza kuwa sekta ya Posta inaendelea kubaki kwenye nafasi ya kipekee ya kuwezesha ukuaji jumuishi kwa kuunganisha watu, biashara na masoko.
Ubia wa kimkakati wa taasisi za serikali, kampuni binafsi zinazotoa huduma za usafirishaji vifurushi, mifumo ya kidijitali, na washirika wa maendeleo, sekta ya posta vinaweza kufungua fursa mpya kwa biashara ndogo na za kati, kuboresha uvumbuzi, na kuwezesha ukuaji wa uchumi wa kidijitali, ameeleza.
Dkt Bakari ameainisha vipaumbele vya TCRA katika kuendeleza sekta ya posta, ambayo imekumbana na changamoto mbalimbali miaka ya hivi karibuni. Hizi ni pamoja na kupungua kwa vitu vinavyosafirishwa chini ya mfumo wa kawida wa utoaji huduma za posta.
Ameeleza kuwa pamoja na changamoto zilizojitokeza, huduma za posta bado ni muhimu sana kwa maendeleo ya Tanzania.
TCRA inaendeleza utunzaji wa mazingira kwa kuhimiza matumizi bora ya njia za kusafirisha vifaa na kutumia vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati kwa ufanisi na ambavyo havitoi hewa chafu. Vilevile inaweka kipaumbele katika upatikanaji wa huduma za posta kwa wote.
Dkt Bakari amesisitiza dhamira ya TCRA kuendeleza ushirikiano wa kikanda na uzingatiaji wa masuala ya pamoja kwenye usimamizi kupitia taasisi za kikanda na kimataifa zinazojihusisha na mawasiliano. Hizo ni pamoja na PAPU, Umoja wa Mawasiliano Afrika Mashariki (EACO) na Chama cha Wasimamizi wa Mawasiliano Kusini mwa Afrika (CRASA).
Ushirikiano huu unawezesha kushinda changamoto zilizoko kipindi hiki na kujenga dunia ambapo ubadilishanaji wa bidhaa na taarifa hautambui mipaka, ameongeza.
Vilevile amewahimiza wadau wengine wa sekta ya posta kuwezesha huduma za posta kuwa za kiubunifu zaidi, salama, za kuaminika, nafuu na zinazofaa wananchi.