TCRA yawezesha Ukuaji wa Sekta na Mfumo Shirikishi

Na Mwandishi Wetu
SEKTA ya Mwasiliano Tanzania imeshuhudia ukuaji mkubwa ndani ya miaka miwili iliyopita, hali iliyochangiwa kwa kiasi kikubwa maboresho ya Sheria na utendaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Ukuaji huo ni pamoja na kuenea huduma miongoni mwa wananchi na maeneo mengi zaidi Tanzania na kujengeka kwa mfumo shirikishi kwenye huduma za kidijitali.
Takwimu za hivi karibuni za hali ya mawasiliano Tanzania, zilizotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt Jabiri Bakari zinaonesha kuwa laini zinazotumika kwa simu za mkononi zilifikia milioni 92.7 Juni mwaka huu, ambapo milioni 54.1 zilitumika kupata huduma za intaneti.
Takwimu hizo zinaonesha ongezeko la laini milioni 2.5 kati ya Machi na Juni 2025, kutoka milioni 90.2 hadi hizo milioni 92.7.
Matumizi ya intaneti na vifaa vya kisasa yaongezeka
Huduma za intaneti zimeenea miongoni mwa watu Tanzania kwa asilimia 79, hali inayoashiria kuwa lengo la serikali la asilimia 80 ifikapo mwisho wa mwaka huu litafikiwa.
Simu zenye uwezo mkubwa, maarufu kama simu janja zimeenea kwa asilimia 37 miongoni mwa watu Juni 2025, kutoka asilimia 25 mwaka 2022.
Kuwepo kwa laini za zaidi ya idadi ya watu Tanzania inatokana na watumiaji kuwa na zaidi ya laini moja. Hii inatokana na mahitaji ya huduma nyingi za kidijitali.
Dkt Bakari anaielezea hali hii kuwa inaonesha kuwa watu wengi zaidi, hasa vijana, wakiwemo wanafunzi na wajasiriamali sasa wanapata huduma za kidijitali za aina mbalimbali na sio tu kwa ajili ya maongezi.
Anaongeza kuwa intaneti inawezesha ujifunzaji na biashara kupitia mitandao.
Mitandao imara, kasi ya mawasiliano
Dkt Bakari anaelezea namna teknolojia za mawasiliano ya simu za mkononi uzao wa tatu (3G), na wa nne (4G) na wa tano (5G) zinavyoenea kwa kasi Tanzania. Hadi Juni 2025, 3G na 4G zilienea miongoni mwa watu kwa asilimia 93 na 92 mtawalia.
Laini za 5G ziliongezeka kutoka milioni 1.19 Aprili 2025 hadi milioni 1.31 Juni mwaka huu. Teknolojia hii ilienea kijiografia kwa asilimia 26, kutoka 23 kipindi hicho.
Wachambuzi wanaeleza kuwa maendeleo haya yanaonesha namna Tanzania inavyokwenda na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani.
Dkt Bakari ana matumaini makubwa kuwa huduma zinazowezeshwa na teknolojia za 4G na 5G zitawezesha Tanzania kupiga hatua kubwa kwenye matumizi ya mifumo ya kidijiti kutoa huduma za uendeshaji serikali, tiba na fedha.
Pesa kwa simu zawezesha ushiriki wa wengi
Ushiriki wa watu wengi kwenye mfumo wa fedha kidijitali umetokana na msukumo wa kiusimamizi unaofanywa na TCRA.
Akaunti za pesa kwa simu zimeongezeka maradufu ndani ya miaka mitano: kutoka milioni 25.8 mwaka 2019 hadi milioni 68.1 Juni 2025.
Hii imewezesha wajasiriamali wengi, wakiwemo vijana kufanikisha shughuli zao kwa kupata fursa za kifedha ambazo walizikosa kupitia mifumo ya kawaida ya kibenki.
Kuwezesha vijana
Pamoja na mafanikio haya kwenye kuenea huduma, TCRA imewekeza katika mpango wa klabu za kidijitali kwenye shule na vituo vya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA). Aidha, inawashirikisha watengenezaji maudhui na program tumizi mbalimbali zinazolenga kujenga uelewa wa masuala ya kidijitali.
Mipango ya TCRA, ikiwemo ya kuendeleza uvumbuzi imewapatia Watanzania wengi nyenzo za kuingia kwenye ujasiriamali kupitia fursa za kidijitali.
TCRA inahimiza mara nyingi kuwa ujenzi wa uchumi wa kidijiti Tanzania unategemea Watanzania wanaowezeshwa kuvumbua na kuongoza.
Kupunguza tofauti za hali ya mawasiliano
Maeneo ya vijijini na jamii zisizo na fursa za kupata huduma yamefikiwa kupitia mipango ya kujenga minara na kuweka vifaa vya mawasiliano ya simu za mkononi vijijini.
Mipango hii inatekelezwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), ambamo TCRA inashiriki.
Miradi iliyotekelezwa na UCSAF imewezesha kupatikana huduma za simu za mkononi kwa maongezi na intaneti kwenye vijiji vingi. Imewezesha upatikanaji wa huduma za afya na tiba na biashara mtandao kwa wananchi wengi zaidi.
Mwelekeo na matarajio
Pamoja na uwezo wa kumilki vifaa vya mawasiliano na vifurushi vya data kuwa na changamoto, wachambuzi wanaona kuwa Tanzania iko kwenye njia sahihi ya ukuaji.
Msimamizi anatakiwa kuendeleza mkazo aliouweka kwenye mikakati ya kuunganisha watu wengi zaidi na kuhimiza upatikanaji wa vifaa vya kisasa. Kueneza stadi za kisasa za kidijitali pia ni muhimu.
Kwa viwango hivi vya kuenea miundombinu na huduma, kuongezeka ubora na watu wengi zaidi hasa vijana kupata huduma za kidijitali, Tanzania inafuata dira yake kwa usahihi kuelekea uchumi shirikishi unaotegemea TEHAMA na mifumo ya kidijitali.