JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Teknolojia Kuboresha Maombi ya Leseni Huduma za Mawasiliano


Teknolojia Kuboresha Maombi ya Leseni Huduma za Mawasiliano

 

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeanza kutumia Mfumo ulioboreshwa unaohusisha kupokea maombi ya leseni kwa kundi la Leseni kubwa. Mfumo huo unamuwezesha muombaji wa leseni kuwasilisha maombi yake bila kulazimika kufika katika ofisi za TCRA.

Mfumo huo laini wa maombi ya leseni (License Management System-LMS) uliozinduliwa siku ya Jumamosi Tarehe 31 Julai mwaka huu na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile (Mb) akiwa sambamba na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Innocent Bashungwa utarahisisha upatikanaji leseni za Mawasiliano na kuongeza tija katika uwekezaji kwenye sekta ya Mawasiliano.

Aidha mfumo huo unaopatikana kwenye tovuti ya TCRA www.tcra.go.tz utasaidia kuongeza ufanisi wa upatikanaji leseni kwa wateja wanaonuia kutoa huduma za Mawasiliano na utangazaji, utaokoa muda wa muombaji leseni, utaokoa gharama za ufuatiliaji kwa mwombaji mpya wa leseni au anaetaka kuhuisha leseni yake, utaongeza ufanisi kwa pande zote mbili yaani Mamlaka inayotoa leseni na mwombaji, utaongeza uwazi kwa kuwa utamwezesha mwombaji wa leseni kupata mrejesho moja kwa moja kwenye simu yake ya kiganjani au kupitia barua pepe juu ya hatua zote na maendeleo ya uchakataji wa leseni aliyoomba na kumwezesha mwananchi anaeomba leseni kuendelea na shughuli za maendeleo badala ya kufuatilia leseni.

Makundi ya leseni yanayopatikana kwenye mfumo huu ni pamoja na Leseni za pamoja ikihusisha leseni za Huduma ya Maudhui (Content Services), Huduma ya Mtandao (Network Services), Huduma ya Mifumo Tumizi (Application Services) na Miundombinu ya Mtandao (Network Facilities).

Leseni nyingine ni Leseni ya Huduma za Vifurushi na Vipeto, Leseni ya Mtumiaji wa Masafa, Leseni ya Matengenezo na Usimikaji, Leseni ya Uagizaji Nje na Usambazaji, Rasilimali za Utoaji Namba, Leseni ya Huduma za Posta kwa Umma na Leseni ya Vifaa Vilivyoidhinishwa.

Hatua ambazo mwombaji wa leseni husika atapaswa kufuata ni pamoja na kutembelea tovuti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambayo ni www.tcra.go.tz kisha kugonga kiunga cha Utoaji Leseni na kisha kubofya kiunga cha Mfumo wa Kuomba leseni ambacho kitampeleka moja kwa moja kwenye ukurasa wenye fomu za kujaza ili aweze kupatiwa leseni anayohitaji kwa ajili ya kutoa huduma za Mawasiliano.

Awali ya yote kabla ya mwombaji kuendelea na maombi ya leseni atatakiwa kujisajili kwa kuweka anuani ya barua pepe na nywila katika sehemu ya mfumo wa maombi ya leseni kisha ukurasa wenye fomu-laini utafunguka ili ajaze nafasi zilizo wazi na kupakia dokyumenti zinazohitajika. 

Hatua za maombi ya leseni za Mawasiliano kwa kundi la leseni kubwa (Individual License) zitasalia kama ilivyokuwa awali ambapo baada ya mwombaji kuwasilisha maombi yake kupitia Mfumo wa Maombi ya Leseni, itafuata hatua ya kutoa tangazo kwa umma ili kualika maoni ya wananchi juu ya mwombaji leseni, kisha tathmini itafanyika juu ya ombi lililowasilishwa, mwombaji kualikwa kutoa wasilisho la huduma ya Mawasiliano anayotarajia kuitoa na kisha hatua ya uidhinishaji leseni na hatimae mteja kupatiwa leseni.

Hatua hii inakuja ikiwa ni mkakati wa serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kurahisisha utaratibu wa upatikanaji huduma za leseni na kuweka mazingira rafiki zaidi kwa wawekezaji katika sekta ya Mawasiliano, sekta ambayo inatoa mchango chanya katika ukuaji wa maendeleo ya taifa.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!