JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Wajumbe wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Watembelea TCRA


Wajumbe wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza...

Dar es Salaam, 20 Novemba 2023 - Wajumbe wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar wametembelea Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa lengo la kujifunza na kupata uzoefu wa namna TCRA inatekeleza majukumu yake, mafanikio yake pamoja na mipango ya utatuzi wa changamoto za sekta ya mawasiliano.

Ziara hiyo iliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Yahya Rashid Abdulla, ikiwahusisha wajumbe saba kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Wajumbe hao mara baada ya kuwasili TCRA makao makuu walipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri Bakari, ambaye aliwapa wasilisho kuhusu shughuli zinazosimamiwa na TCRA, pamoja na mafanikio na changamoto zinazokabili sekta ya mawasiliano nchini na namna Mamlaka hiyo ilivyojidhatiti kuzikabili.

Katika wasilisho lake, Dkt. Bakari alitaja mafanikio ya TCRA katika usimamizi wa sekta ya mawasiliano kuwa ni pamoja na kupunguza gharama za kupiga simu kwenda mitandao mingine, kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za simu na intaneti, na kuimarisha usalama wa mawasiliano.

Wajumbe hao waliipongeza TCRA kwa kazi nzuri inayoifanya katika kusimamia sekta ya mawasiliano nchini. Waliahidi kuendelea kuiunga mkono TCRA katika juhudi zake za kuboresha sekta ya mawasiliano.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Yahya Rashid Abdallah, aliwaasa wataalam wa Mamlaka hiyo kuhakikisha wakati wote wanakuwa mstari wa mbele katika kupokea teknolojia mpya za sekta ya mawasiliano nchini ili kuhakikisha Taifa linakuwa mbele na haliachwi na mageuzi yanayotokea kwa kasi duniani.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!