JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Wakongwe Radio Tanzania (RTD) Watembelea TCRA


Wakongwe Radio Tanzania (RTD) Watembelea TCRA

Na Mwandishi wetu

Umoja wa wakongwe wa Radio Tanzania (RTD) umefika katika ofisi za makao makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) jijini Dar es Salaam kujitambulisha, kuomba ushirikiano na kueleza mikakati ya umoja huo katika kuchangia maendeleo sekta ya utangazaji nchini.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa umoja huo Ally Saidi Tunku wamesema yapo wanayoona wanaweza kuchangia katika tasnia na kujenga jamii bora hasa katika kuendeleza misingi bora ya utangazaji na maadili ya uandishi wa habari.

Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt Jabiri Bakari amesema vyombo vya Habari vina nguvu katika kutengeneza mtazamo wa jamii hivyo bila kuwa na maudhui bora ni rahisi jamii kuenenda vibaya,Amesema TCRA iliandaa  vipindi vya maadili na kuvirusha kupitia vituo mbalimbali vyenye leseni za kiwilaya ikiwa ni kutengeneza jamii yenye maadili.

Dkt. Bakari ameahidi TCRA kutoa ushirikiano kwa umoja huo hasa katika maeneo ya mafunzo ambapo amesema kuna haja kizazi cha sasa katika tasnia ya utangazaji kupata uzoefu wa namna tasnia ilivyokuwa kusudi kuendelea kuyaenzi yale yaliyokuwa mema, amesema wakongwe hao ni hazina kubwa hivyo ni muhimu kuwahusisha katika makongamano na warsha mbalimbali.

Umoja huo wa Wakongwe wa RTD hivi sasa unawanachama 256 na wanajishughulisha na shughuli mbalimbali ikiwemo uandishi wa vitabu hususani vinavyohusu tasnia ya utangazaji kabla na baada ya uhuru na mchango wa Radio katika harakati za ukombozi kusini mwa Afrika.

Miongoni mwa wanachama wa umoja huo waliohudhuria kikao hicho ni Eda Sanga,Godliver Rweyemamu,Judica Losai,Angalieni Mpendu,Ally Said Tunku,Rose Haji Mwalimu,Marie Shaba,Sango Kipozi,Jane Mailleh na Suleiman Kumchaya.

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!