JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAASISI YENYE VIWANGO VYA ISO 9001: 2015

Wakuu wa Shule wahimizwa kuanzisha Klabu za Kidigiti


Wakuu wa Shule wahimizwa kuanzisha Klabu za Kidigiti

Na Mwandishi wetu

Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Maryprisca Mahundi amewahimiza Wakuu wa shule za awali, msingi, sekondari na Vyuo Vikuu kuhakikisha kuwa wanakuwa na klabu za kidigiti mashuleni ili kuhamasiha vijana kuwa na ujuzi wa TEHAMA utakaosaidia kutafuta suluhisho za kiteknolojia za changamoto mbalimbali zilizopo kwenye jamii zinazotuzunguka pamoja na kutumia TEHAMA kukuza Uchumi wa kidigiti ili kujikwamua kimaisha na kuweza kushindana kitaifa na kimataifa.

Mhandisi Maryprisca amezungumza hayo kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wasichana na TEHAMA yaliyofanyika tarehe 25/04/2024 mkoani Arusha ambapo amesema kuwa serikali itaendelea kuunga mkono jitihada zilizopo katika kuongeza idadi ya wasichana wanaochukua masomo ya sayansi na kuwaandaa ili waweze kunufaika vizuri na Uchumi wa kidigiti.

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo yaliyoongozwa na Kauli Mbiu ya “Uongozi” Naibu Waziri Mhandisi Maryprisca ameipongeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania {TCRA} kwa kuratibu Maadhimisho hayo yenye lengo la kuhamasisha Uongozi katika TEHAMA hususani kwa wasichana ili kusogeza ulinganifu wa kijinsia.

Mwenyekiti wa Bodi ya TCRA Dkt. Jones Killimbe amesema anatambua mchango wa wadau mbalimbali katika kuwezesha upatikanaji wa huduma za mawasiliano na kukuza maendeleo ya sekta ya mawasiliano. Ameongeza kuwa ukuaji wa teknolojia unategemea na kuwepo kwa mazingira wezeshi kwa wasichana ili kuendeleza bunifu zao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Jabiri Bakari amesema ni muhimu wasichana kujikita katika utengenezaji wa mifumo na programu za kiteknolojia, kusoma masomo ya uhandisi, kujikita katika tafiti za teknolojia mpya kama Akili Mnemba (Artificial Intelligence- AI) na kuwa sehemu ya wataalamu wa masomo ya TEHAMA wa ngazi zote za elimu na baadae kushiriki kwenye kutunga sera hasa katika eneo hilo la TEHAMA.

Dkt. Jabiri amesema takwimu zinaonyesha kukua kwa kasi kwa sekta ya mawasiliano nchini ambapo hadi kufikia mwezi Machi, 2024 kumekuwa na laini za simu milioni 75 kutoka laini za simu milioni 61 mwezi Juni mwaka 2023 ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 13. Aidha takwimu za Machi pia zinaonyesha kuongezeka kwa watumiaji wa intaneti kwa asilimia 8.3 kutoka watumiaji milioni 34 mwezi Juni mwaka 2023 hadi kufikia milioni 36.8 mwezi Machi mwaka 2024.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA ametaja baadhi ya sababu zinazochangia ongezeko hilo kuwa ni matumizi ya intaneti ambayo pia yamechangia kuwa na maudhui mengi ya Kiswahili, uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu umefanyika kwenye teknolojia zote yaani 2g, 3g, 4g na 5g. Pia teknolojia ya huduma za intaneti kwa kutumia Nyaya yaani fiber imechangia kuongezeka kwa matumizi ya intaneti ambapo takribani watumiaji elfu 49 wananufaika na teknolojia hiyo majumbani (Fiber To Home) huku watumiaji zaidi ya elfu 5 wakinufaika na teknolojia hiyo maofisini (Fiber To Office)

Pia Takwimu za utangazaji zinaonyesha kumekuwa na ongezeko la ving’amuzi na ongezeko la watoaji huduma za maudhui mtandaoni huku huduma za Posta na usafirishaji wa vipeto zikiwa zimeongezeka na hivyo kuchagiza ukuaji wa biashara mtandao yaani ecommerce.

Kuhusu ubora wa huduma za mawasiliano Dkt. Jabiri amesisitiza ni kutokana na jitihada zilizofanywa na serikali kwa kushirikiana na watoa huduma katika kuboresha  huduma za posta, utangazaji, simu na intaneti kwa kuwa ni muhimu katika kuleta maendeleo ya taifana kuchangia kuimarika kwa miundombinu ya kidigiti na kuchangia kwenye ukuaji wa kiuchumi. Ameongeza kuwa TCRA itaendelea kutoa taarifa za mwenendo wa ukuaji wa sekta ya mawasiliano kila baada ya miezi mitatu ili wadau waweze kuwa na uelewa wa pamoja wa ukuaji wa sekta hiyo.

Akitoa salamu za Naibu Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bwana Elisa Mbise amesema Wizara kupitia TCRA itaendelea kuweka mazingira bora ya kukuza TEHAMA ambapo tayari ipo kwenye mchakato wa kuboresha sera ya TEHAMA ili iandane na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Nae Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Arusha  Felician Mtahengerwa amewashauri wasichana kutumia TEHAMA vizuri kwa kujijenga kiakili ili kupata ujuzi utakaowawezesha kushindana kwenye ngazi mbalimbali ulimwenguni na kuhamasisha wasichana kuchukua masomo ya sayansi kwa kuwa Taifa bado lina uhitaji mkubwa wa wataalamu wengi haswa wa jinsia ya kike katika masuala ya teknolojia na TEHAMA.

Maadhimisho hayo pia yaliambatana na maonyesho ya kazi mbalimbali za wanafunzi zinazoonyesha suluhisho za kiteknolojia za changamoto zilizopo kwenye jamii ya Tanzania. Akizungumza akiwa kwenye maonyesho hayo Naibu Waziri Mhandisi Maryprisca Mahundi ametoa rai kwa TCRA kuhakikisha kuwa kunakuwa na utaratibu mzuri wa wabunifu hao kupata haki ili wanafunzi waweze kunufaika na suluhisho walizobuni ikiwa ni pamoja na kujitengenezea ajira.

Aidha Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Jabiri Bakari alisema kuwa Mamlaka ya Mawasiliano kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) inaunga mkono kazi za ubunifu wa kiteknolojia kwa kutoa rasilimali za mawasiliano zinazohitajika bure kwa kipindi cha miezi mitatu ili kuwawezesha na kuinua bunifu zao.

Maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Wasichana na TEHAMA huadhimishwa kila Alhamisi ya mwisho wa Mwezi wa Aprili kwa lengo la kuhamasisha wasichana kuchukua masomo ya sayansi. Siku hiyo inatokana na makubaliano ya nchi wanachama wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya TEHAMA (International Telecommunications Union - ITU). Kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka 2024 ni “Uongozi”

Je, una Maswali yoyote juu ya Sekta ya Mawasiliano?
Tuma Mrejesho na Malalamiko!

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja na wadau wake wote.

Tuma Mrejesho na Malalamiko!